
BAADA ya Rais Dk. John Pombe Magufuli ‘JPM’ kuliamuru Baraza la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) wataalamu wake wapime mara moja maji yote yanayotumiwa kuoga, kunywa wanachi na mifugo yao katika vyanzo vyote ya maji katika vijiji vinavyozunguka mgodi wa dhahabu wa North Mara, Nyamongo, Wilaya ya Tarime, Mkoa wa Mara, simulizi ya vifo eneo hilo inatisha.
Magufuli alipata kero hiyo aliposimamishwa na wananchi walipompokea na mabango yao eneo la Kwinogo Kijiji cha Kewanja, Kata ya Kemambo, Nyamongo yaliyoandikwa ujumbe mbalimbali kubainisha adha wanazozipata wakazi wa eneo hilo tangu mgodi huo uwekezwe na makampuni ya kigeni yaliyochimba na yanayoendelea kuchimba dhahabu maeneo hayo, hivyo na gazeti hili kuamua kufuatilia athari zinazodaiwa kutokea kwa wananchi.
WALIOFARIKI DUNIA
Wakati Rais Magufuli anachukua hatua hiyo, gazeti hili limepata simulizi ya kutisha kwa kuarifiwa kuwa tayari baadhi ya watu wamedaiwa kufariki dunia kwa nyakati tofauti kutokana na kuoga au kunywa maji yenye sumu. Wenyeji wamewataja watu hao waliofariki dunia kuwa ni Mwita Mwikwabe Waigama, Japipo Jeradi, Magaigwa Mang’era Kirindo na mtoto Ayubu Daniel Mohere.
“Hifo hivyo vinatusikitisha na mbaya zaidi, hakuna msaada wowote kutoka serikali licha ya sisi kulia sana, tumshukuru rais kwa kuliona hili,” alisema Mwita Mwita, mkazi wa eneo hilo.
HAWA WANATESEKA
Baadhi ya watu ambao wanadai bado wanateseka na maradhi kutokana na maji hayo yenye sumu baada ya kunywa au kuoga ni pamoja na Boazy Range Isaroche, Esther Mugusuhi, Anastazia Mwita, Debora Marwa Byanda ambao pamoja na juhudi zao za kujua ukweli wa maradhi wanayoyaugua ziligonga mwamba kila walipohitaji ukweli wa kilichosababisha maradhi yao hayo na kila mmoja anadai hawakupatiwa ukweli huo kutokana na mtandao unaokinga na kulinda maji yanayotiririka na kuwafikia wananchi kuficha ukweli.
SAKATA LILIFIKA MAHAKAMA KUU
Madhara ya maji hayo yaliipata familia na Chacha Kiguha na mkewe Neema Chacha na watoto wao Bhoke, Kiguha, Motongori na Surati Chacha Kiguha ambao waliamua kwenda mahakamani katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza na kushinda madai yao ya madhara yanayotokana na maji kutoka kwenye mgodi huo Agosti 2016.
Licha ya mgodi huo kukata rufaa mahakama ya rufaa kupinga hukumu hiyo, mgodi huo ulishindwa na uliamuliwa uilipe fidia familia hiyo kutokana na kesi ya madai ya madhara uliowasababisha. “Ni kweli maji haya ya sumu yana madhara makubwa kama unavyoona watoto na wazee, wanababuka miili na kufa kama unakunywa au kuoga. Mifugo pia inakufa,” alikiri Chacha Kiguha akiwa na mkewe, Neema.
Wakazi wa eneo hilo wanadai kuwa maji ya sumu kutoka katika bwawa la maji la mashimo ya Gokona na Nyabigena yalipoingia katika Mto Tighite na kusambaa katika visima na vyanzo vya maji vya asili walivyovitumia kwa kunywa, kuoga na kunywesha mifugo yao tangu mwaka 2008, wengi wamepata madhara.
“Madhara hayo bado yanaendelea baada ya Serikali na mgodi kushindwa kuchukua hatua hadi sasa za kuwanusuru wananchi wa vijiji hivyo na mifugo yao na sasa wanaoathirika na maji hayo wanazidi kuongezeka wakati wale wa kipindi hicho hawajapona afya zao,” alisema mwananchi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la John Okea.
PROFESA MUHONGO
Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliwahi kukataa taarifa ya NEMC alipotembelea vijiji hivyo na kuamua kuchukua sampo za maji hayo baada ya kuingiwa na huruma alipojitokeza mbele yake mama wa mtoto Ayubu Daniel Mohere, Neema Daniel Mohere, Februali 12 mwaka 2016 mwanaye akiwa na hali tete na mama huyo akadai kuwa amepata madhara ya maji ya mgodi huo baada ya kumuogesha.
Mtoto huyo licha ya mama yake kuonesha juhudi za kuokoa maisha yake alifariki dunia Machi 25 mwaka 2017 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya KCMC na alizikwa Machi 27 mwaka 2017 hukohuko katika viwanja vya hospitali baada ya mama huyo kukosa uwezo wa fedha za kuusafirisha mwili huo kuja kuuzika Nyamongo.
Mwandishi wetu alishuhudia Profesa Muhongo, akichukua sampo ya maji hayo yanayodaiwa kuwa na sumu akadai anayapeleka nchi za Ufaransa, Ubelgiji na Ujeruman kupimwa Julai 18 , 2016 baada ya kuikataa taarifa ya NEMC iliyosomwa juu ya vipimo vya maji hayo mbele yake ikisema kuwa maji ni safi na salama bali wananchi hao wanaugua magonjwa mengine na mifugo ya familia ya Mang’era Nyamboge Ntora iliyokufa kwa madai kunywa maji ya sumu ya kutoka mgodini siyo sahihi.
Hata hivyo, Profesa Muhongo alikwama hadi anaondolewa uwaziri hakuwahi kurejesha majibu ya vipimo vya maji hayo licha ya kufanya ziara na kuzungumza na wananchi wa vijiji vinavyozunguka mgodi huo Februali 10, 11 na 12 mwaka 2016 kisha akaunda kamati yake ya watu zaidi ya 25 kuchunguza matatizo ya mgodi na wananchi aliyoipatia siku 30 kukamilisha.
Taarifa za awali ya mwaka 2014, iliyotolewa kwa wananchi ilisema maji hayo yana sumu na ilipendekeza yasitumika kwa watu na mifugo na kushauri mgodi huo uwahamishe watu na mifugo yao waliopo karibu karibu na mgodi huo kuepuka madhara hayo lakini baadhi ya wana vijiji hawakutekelezewa hivyo.
Mbali na taarifa hiyo, taarifa ya familia ya marehemu Ntora waliyoipeleka sampo za mmoja wa ng’ombe 168 waliokufa kwa kunywa maji hayo katika maabara ya nchini Kenya ilithibitishwa kwa kuidhinishwa na mkemia wa serikali ya nchi hiyo mwaka 2015 kuwa maji hayo yana sumu wakati sampo hizo hizo walipozipeleka katika maabara ya Tanzania Kanda ya Mwanza mwaka 2015 hawakuona sumu yoyote ile.
Haikuwahi kutolewa taarifa ya ukweli wa maji hayo na Serikali tangu kulipozuka sakata hilo lakini sasa Rais Magufuli amecharuka na kutaka maji hayo yachunguzwe upya na ripoti yake itolewe kwake na wataalamu wa NEMC jambo ambalo wananchi wanasema ni ukombozi mkubwa kwao kwani ukweli utajulikana.
Rais alisema kuwa pamoja kuwa anawaagiza wataalam wa NEMC anazo taarifa sahihi za maji hayo kuwa yana sumu na yametumika kuwaua baadhi ya watu na wengine wameendelea kuathiriwa bila kupona wakiugulia majumbani baada ya kukosa uwezo bila kusaidiwa matibabu yao na mgodi huo.
“Kwa muda mrefu nimekuwa nikifuatilia sakata hili kwa kuwa mimi pia ni mkemia kabla ya kuwa rais wa nchi,” alisema Magufuli.
STORI: IGENGA MTATIRO, UWAZI