



MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo amezindua rasmi zoezi la utambuzi na usajili kwa watu wenye ulemavu ili waweze kupata vitambulisho vya utaifa ambavyo vinatolewa na Mamlaka ya Vitambulisho Vya Taifa (NIDA) na idara ya ustawi wa jamii.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Chongolo ameipongeza mamlaka hiyo na idara ya ustawi wa jamii Kinondoni kwa kuwajali watu wenye mahitaji maalumu na kuandaa jukwaa la kuwatambua na kuwasajili na kutoa vitambulisho.
Amesema kuwa vitambulisho hivyo vitawasaidia katika kupata huduma mbalimbali ya kijamii na amewataka wanajamii kuwahimiza na kuhakikisha kila mtu mwenye ulemavu wa aina yoyote anapata huduma hiyo ya utambuzi na usajili na kupatiwa kitambulisho chake cha utaifa.
Kwa upande wake Ofisa Msajili (NIDA) Wilaya ya Kinondoni, Dickson Mbanga amesema kuwa mchakato wa utoaji wa vitambulisho kwa walemavu umekuwa na changamoto kubwa hivyo kama mamlaka kwa kushirikiana na ofisi ya mkuu wa Wilaya wameweka mazingira rafiki ya kuwasajili watu wenye ulemavu na wajiatie vitambulisho vya utaifa.