BAADA ya juzi Jumamosi Simba kubanwa na Ndanda, kocha mkuu wa kikosi hicho, Patrick Aussems, raia wa Ubelgiji, ameibuka na kusema kuwa, kama viwanja vingine vya mikoani vitakuwa na ubora wa chini kama ilivyo kwa Nangwanda Sijaona, basi kuna hatari kwao ya kupata ushindi.
Kauli ya Aussems imekuja muda mfupi baada ya kukishuhudia kikosi chake kikishindwa kufungana na Ndanda katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa juzi Jumamosi kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.
Kabla ya mchezo huo wa juzi, Simba ilicheza uwanjani hapo dhidi ya Ndanda mara nne na kushinda mechi zote, lakini juzi Jumamosi kwa mara ya kwanza imeshindwa kupata ushindi, huku Aussems akiulalamikia uwanja kutokuwa na ubora.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Aussems alisema: “Kama kutakuwa na viwanja vingi vya aina hii, basi itakuwa tatizo kubwa kwetu kupata ushindi tukienda kucheza huko. Uwanja huu hauna ubora kabisa.
“Nawapongeza Ndanda kwa kupata sare hii kwani tangu mwanzo wa mchezo wao waliingia wakiwa na nia ya kujilinda zaidi kuliko kushambulia na wakafanikiwa kwa hilo. Hivi sasa tunajipanga kuangalia tunapata matokeo mazuri katika mechi zijazo.”
Simba baada kucheza na Ndanda juzi, Alhamisi ijayo itakuwa Mwanza kupambana na Mbao FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, kisha itaenda Shinyanga kucheza na Mwadui kwenye Uwanja wa Kambarage.
Sweetbert Lukonge, Mtwara