SINGIDA: Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Rehema Nchimbi amepiga marufuku uanzishwaji wa kumbi za starehe zenye kujihusisha na vitendo vya ukahaba vinavyosababisha mipira ya kiume kuzagaa eneo la shule. Marufuku hiyo aliitoa hivi karibuni wakati akizungumza na watendaji walio chini yake ofisini kwake.
“Hivi karibuni niliifunga baa moja ya usiku iliyopo karibu na Shule ya Msingi Ipembe kutokana na mambo machafu yanayofanywa kwenye baa hiyo usiku. “Hatuwezi kuwa na baa zinazokumbatia matendo machafu usiku halafu watoto wetu wakiamka wanakuta mipira ya kiume (Kondomu) imezagaa kwenye viwanja vyao.
“Tunajenga jamii ya aina gani? Hata nilipoifunga baa hiyo ya usiku nilikuwa nalinda maadili ya watoto wetu, lakini mwenye baa alikimbilia mahakamani akapewa ruhusu ya kuendelea na biashara yake, jambo ambalo limenihuzunisha,” alisema Dk. Rehema. Aliongeza kuwa hataki kuzungumzia kuhusu hukumu hiyo ya mahakama kwa sababu ya kutotaka kuingilia uhuru wa chombo hicho cha kutafsiri sheria, lakini alisisitiza kwamba lazima hatua ya kupiga marufuku uwepo wa baa za aina hiyo zichukuliwe.
Aidha, mkuu huyo wa mkoa aliwaagiza viongozi wa manispaa kuacha mara moja kukusanya kodi kwa wamiliki wa kumbi za starehe zinaharibu mila na desturi za nchi na kuwataka watafute mapato kwa njia nyingine. “Usiku kuna vitu vya ajabu, mimi nina ‘klipu’ za mambo ambayo yanafanyika kwenye baadhi ya kumbi za starehe na baa …wazee wangu niwambie kuna siku kulikuwa na akina baba watatu walikuwa wanamfukuza msichana ambaye hana nguo.
“Wanamfukuza kama mbwa, walimfukuza wakaja kumkamatia pale barabarani yaani walichomfanyia ni aibu hata kueleza.“Sasa mimi siwezi kuvumilia mambo haya ya ovyo kwani siyo sera wala ilani ya uchaguzi ya CCM (chama kinachoongoza serikali). “Ni kweli kwamba tunahitajika uwekezaji, lakini siyo wa aina hiyo utakaofanya malezi ya watoto wao yasiwe sawa, nalisema hili
kwa ukali,” alisema mkuu huyo wa mkoa. Katika hatua nyingine wananchi wamepongeza hatua hiyo ya Dk. Rehema ya kupiga marufuku kumbi za starehe zinazokiuka maadili na kumuomba kiongozi huyo wa serikali aendelee kupambana na tatizo hilo hadi mwisho.
STORI: Jumbe Ismailly, Risasi Mchanganyiko