×

Wachezaji Wawili Simba Wawekwa Pembeni

Kocha Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma.

 

WACHEZAJI kadhaa walioachwa wakifanya mazoezi na Kocha Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma Jijini Dar es Salaam, huenda wakaikosa mechi dhidi ya Yanga Septemba 30 kama Patrick Aussems akishikilia msimamo wake.

 

Kocha huyo raia wa Ubelgiji ameiambia Spoti Xtra kwamba; “Nimefurahi kuwaona wachezaji Niyonzima(Haruna) na Juuko(Murshid) ni wachezaji niliokuwa nawasikia, kama unavyofahamu hao ni wachezaji wapya kwangu na ukiangalia tayari nina wachezaji niliokuwa nao muda mrefu katika timu ambao tayari wamezoea na kuushika mfumo wangu.

 

“Hivyo, ninahitaji muda wa wiki tatu kwa ajili ya kuwaangalia na kuwaingiza katika mfumo mpya ninaoutumia, hivyo siyo kazi kuushika mfumo inahitaji muda kuuelewa,”alisema Aussems ambaye timu yake inacheza na Mbao leo Mwanza.

Wachezaji wengine walioachwa na Masoud ni pamoja na Asante Kwasi, Hassan Dilunga, Said Nduda na Muzamiru Yasin.

 

Manara amvaa Djuma

Msemaji wa Simba, Haji Manara amemvaa Masoud Djuma; “Kumekuwa na posti nyingi mitandaoni pamoja na matusi ambayo natukanwa, kisa suala la Djuma, nimempigia simu kocha na kumueleza tabia ya mashabiki wa Simba ambapo mara nyingi wamekuwa wakibadilika wanaweza kumtetea sasa na baadae wakamgeuka.”

 

“Awali walisema kuwa kocha huyo ni mdogo kuweza kukabidhiwa jukumu la kuiongoza timu hiyo, lakini tulikuwa nae katika michuano ya Kagame tulifungwa fainali na Kagere, Mapinduzi Cup pia tulifungwa, hivyo ni maamuzi ya kocha hatuwezi kumzuia lengo likiwa ni kujenga.”

Okwi na Bocco

Aussems juzi Jumatatu jioni alitumia dakika 15 kufanya kikao na washambuliaji wake Mganda, Emmanuel Okwi na John Bocco.

Kikao hicho kilitumia dakika 15 tangu walipoanza saa 12:00 hadi 12:15 jioni wakiwa wamesimama ndani ya uwanja wa Boko Veterani huku akizungumza nao kwa ishara za mikono.

 

Alipoulizwa na Spoti Xtra kuhusiana na kikao chao alisema kuwa; “Hawa ni vijana wachezaji wangu tena nawachukulia kama watoto wangu. Nilikuwa nawasahaulisha na matokeo tuliyoyapata mechi na Ndanda.”

HABARI NA WILBERT MOLANDI

SPOTI XTRA ALHAMISI LAANZA KWA KISHINDO