×

Mume Akiri Kumuua na Kumfukia Mkewe, Mwili wa Wafukuliwa

MWILI wa marehemu Celina Sulubu, mkazi wa Lubambawe wilayani Mkuranga, mkoani Pwani umefukuliwa kwa taratibu za kisheria baada ya mumewe Selemani Hija Usumba kukiri kwamba alimuua mkewe huyo kisha kumfukia.

 

Usumba inadaiwa kwamba, Septemba 21, mtuhumiwa alifika Kituo cha Polisi Mkuranga na kuripoti kuwa mkewe Celina ametoweka nyumbani kwake tangu Septemba 13 mwaka huu.

 

Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kipolisi Rufiji ,Onesmo Lyanga amesema baada ya kupokea taarifa hiyo mkuu wa upelelezi wilaya ya Mkuranga alifungua jalada la uchunguzi na kumshikilia kwa mahojiano na uchunguzi zaidi ambapo katika mahojiano ya awali alikiri kumuua mkewe kwa kumkaba shingoni na kumsababishia kifo mkewe.

 

Baada ya kutenda kitendo hicho alichimba shimo kwenye shamba la jirani ambalo alikabidhiwa kulilinda na kisha kumzika.

 

“Septemba 22 mwaka huu, timu ya makachero ikiongozwa na mkuu wa upelelezi wilaya ya Mkuranga pamoja na mashahidi mbalimbali wa tukio hili walifika eneo la tukio kwa kuongozwa na mtuhumiwa ” alisema Lyanga na kuongeza kwamba baada ya kufika eneo hilo mtuhumiwa alionyesha alipouzika mwili wa marehemu ambapo ulifukuliwa kisheria.

 

Baada ya kufanyiwa uchunguzi, mwili wa marehemu ulikabidhiwa ndugu kwa ajili ya mazishi huku uchunguzi zaidi ukiendelea.

BREAKING: MAGUFULI AAGIZA KIVUKO KIPYA KITENGENEZWE HARAKA