MIONGONI mwa vilele vya shamra na “maraha ya kufa mtu” vilivyojiri siku ya kuzaliwa mwigizaji nguli Bongo, Wema Sepetu, ambayo ilifanyika jijini Dar es Salaam usiku wa Septemba 28, ni pale mama yake alipojibu kiaina swali aliloulizwa na mwanahabari kuhusu alivyojisikia pale bintiye alipoondoka kwenda kushiriki uigizaji filamu huko Ghana.
“Wema katimiza miaka kumi na nane, tusikerane bwana!” alijibu mama huyo akimaanisha kwamba bintiye ni mtu mzima hivyo hakuwa na sababu ya kuingiwa na wasiwasi wowote kuhusu kuondoka kwake.
Katika hafla hiyo, Mama Wema alisema alifika kumsapoti mwanaye huyo kipenzi pamoja na kwamba alikuwa anaumwa, lakini akiwa mzazi aliona faraja kwa mwanaye kupiga hatua na kufanya kazi na wasanii wakubwa wa kimataifa akiwemo Raia wa Ghana, Van Vicker.
Aidha, alisema hayupo tayari kuulizwa maswali aliyoyaita ya kukera kwani alikwenda kwenye hafla hiyo ili afurahi na badala yake aliwataka wanahabari kumwuliza maswali ya maendeleo na yenye kumfariji mwanaye.
Hafla ya kusheherekea siku yake ya kuzaliwa ilifanyika katika ukumbi wa Mlimani City ambapo siku hiyo pia alizindua filamu yake ya ‘Day After Death’ ambayo ameshirikiana na Van Vicker mwigizaji nguli kutoka Ghana.