
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, linawashikilia watu zaidi ya 60 kwa tuhuma za kufanya uhalifu na kuharibu miundombinu ya shirika la umeme nchini, TANESCO.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuhusu oparesheni za jeshi lake, Kamanda wa Polisi Kanda ya Dar es Salaam, SACP Lazaro Mambosasa, amesema miongoni mwa matukio mengine ya uhalifu ni lile linalomhusu mwendesha bodaboda, Matthew Joseph, anayedaiwa kumiliki bunduki aina ya Shot Gun kinyume cha sheria na kuitumia bunduki hiyo kufanyia uhalifu.
Katika hatua nyingine, Mambosasa amesema kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Dar es Salaam kimekusanya zaidi ya Sh. bilioni mbili kutokana na makosa mbalimbali ya barabarani.