
Timu ya Yanga itamkosa kocha wake, Mwinyi Zahera, siku ya Jumapili dhidi ya Mbao FC katika Uwanja wa Taifa.
Msemaji wa Yanga, Dismas Ten amesema Zahera hatakuwepo nchini kwa kuwa ataungana na timu ya taifa lake ya DR Congo itakayokuwa ikipambana kuwania kucheza Kombe la Mataifa Afrika (Afcon).
“Kwa hiyo kocha hatutakuwa naye, lakini kila kitu kipo katika mpangilio na vijana wako tayari kwa kuwa wamekuwa na kocha muda wote,” alisema.
Zahera bado ni kocha msaidizi wa timu ya taifa ya DR Congo na mmoja wa makocha wazalendo wa nchi hiyo wanaoaminika.
Pia msemaji huyo wa Yanga amesema wameandika barua kwenda Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kitendo mchezaji wa Simba, James Kotei kumpiga Gadiel Michael katika mechi ya watani Simba na Yanga, Jumapili iliyopita.
Msemaji wa Yanga, Ten amesema wameamua kufanya hivyo kama klabu wakionyesha wamekerwa na kitendo hicho.
“Kama klabu hatuwezi kukaa kimya kwa vitendo kama hivyo vinatokea, tumeandika barua.
“Sasa tutawaachia TFF wenyewe tuone kama wanachukua hatua au la, lakini sisi tumeonyesha namna tulivyokerwa na vitendo ambavyo si vya kiungwana,” alisema.