
RAIS John Magufuli amesema serikali ya awamu ya tano itaendelea kumuenzi Baba wa Taifa hayati Mwl. Julius Nyerere kwa kuhakikisha fikra na mipango mizuri aliyoiweka inatekelezwa kwa manufaa ya Watanzania.
Magufuli, aliyekuwa amefuatanana mkewe, Janeth, ametoa kauli hiyo leo October 14, 2018 wakati akizungumza na mjane wa Baba wa Taifa, Maria Nyerere, nyumbani kwake Msasani jijini Dar es nSalaam alikokwenda kumtembelea muda mfupi baada ya kushiriki ibada ya misa takatifu ya Jumapili iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Petro, Oyster Bay.
Akisisitiza, Magufuli amebainisha kuwa hayati Nyerere alifanya kazi kubwa ya kujenga misingi imara ya nchi kuwa na amani, umoja na mshikamano na misingi ya uchumi wa kujitegemea kupitia Azimio la Arusha.
Ametoa wito kwa Watanzania wote hasa vijana kuungana na serikali katika kuyaenzi yaliyofanywa na Baba wa Taifa, na pia kuliombea taifa.
Mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere amemshukuru Rais Magufuli kwa kuendelea kumuenzi Baba wa Taifa na amemhakikishia kuwa yeye na wanamaombi wenzake pamoja na Watanzania wote wanamuombea heri yeye, viongozi wote na Taifa kwa ujumla.
Rais na mkewe, walikutana pia na mtoto wa Mwl. Nyerere, Makongoro Nyerere, na wajukuu wa Mwalimu.
Mapema leo asubuhi Rais Magufuli ameungana na waumini wenzake katika Kanisa la Mtakatifu Petro, Oyster Bay jijini Dar es Salaam katika misa takatifu ya kumwombea Mw. Nyerere aliyefariki dunia tarehe 14 Oktoba, 1999.