
GUMZO kubwa kwenye mitandao ya kijamii kwa sasa, ni ishu ya video vixen anayechipukia Bongo, Lilian Kessy au maarufu kama Kim Nana, kudaiwa kutoka na staa wa muziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’.
Chanzo cha madai haya, ukiachana na ukaribu waliouonesha wawili hawa kwenye ‘birthday party’ ya Diamond, juzikati Diamond aliachia vipande vya video fupi kwenye akaunti yake ya Instagram, vikimuonesha akiwa anaimba wimbo mpya wa msanii aliyepo chini ya Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), Lavalava uitwao Nitake Nini.
Katika video hizo, Diamond anaonekana akipapaswa kifuani kimahaba na mrembo mmoja anayeonekana mkono tu. Ishu ikaanza hapo, mrembo huyo ni nani? Wapo waliosema kwamba ni mzazi mwenzake Diamond, Zarina Hassan ‘Zari The Boss Lady ambaye kwa sasa penzi lao limebaki stori.
Lakini wapo waliodai mkono huo ni wa Kim Nana na wakaweka na ushahidi wa picha za jinsi mkono wa mwanadada huyo unavyofanana na ule unaoonekana kwenye video hiyo. Katika kuchangamkia fursa ya ‘kiki’, Kim Nana naye hakubaki nyuma, akaanza kutupia mafumbo kwenye akaunti yake ya Snapchat, akinukuu baadhi ya maneno ambayo Diamond anasikika akiyaimba kwenye video hiyo! Mambo yakawa ni hiviiii!

Lengo langu siyo kuzungumzia sakata hilo bali nilitaka kidogo kuzungumza na Kim Nana. Namfahamu mrembo huyu kabla hajaanza kujihusisha na hizi kiki. Nimewahi kupata bahati ya kumsikiliza Kim Nana akielezea malengo yake wakati ndiyo anaanza kuandikwa na vyombo vya habari kwa mara ya kwanza. Alijawa na ndoto za kuyabadilisha maisha yake, kupitia sanaa ya u-video vixen na kuibadilisha sanaa hiyo.
Mara kwa mara alikuwa akiwashukia ma video queen wenzake, kwa tabia zao za kupenda kiki, kujirahisi kwa wanaume na kufanya mambo ya hovyohovyo, akieleza kwamba tabia hiyo imekuwa ikifanya kazi ya u-video vixen Bongo, kudharauliwa, jambo ambalo kimsingi ni la kweli.
Mara kadhaa aliingia kwenye vita ya maneno na Amber Lulu na Gigy Money, akiwatuhumu kwamba wanaidhalilisha kazi ya u-video vixen Bongo kutokana na matendo yao. Watu wanaoitakia mema sanaa Bongo, walimuona kama almasi katikati ya vipande vya chupa. Baada ya muda mrefu wa ukimya kupita, hatimaye amerejea tena lakini safari hii, naye ameibuka na mpya, ya kufuata nyayo za yaleyale yaliyokuwa yakifanywa na wenzake waliomtangulia.
Kim Nana anaishi maisha ‘fake’, kazi yake kutwa ni kuposti mapichapicha Instagram, yakimuonesha akiwa anakula bata kwenye viwanja tofautitofauti, kwenye mahoteli makubwamakubwa na kadhalika. Anajiachia na mastaa wakubwa, anatupia picha akionekana kutupia mavazi ya bei kali, akiwa amevaa mawigi ya pesa nyingi na picha nyingine za kihasarahasara mitandaoni akijaribu kuwaaminisha watu kwamba maisha yake ni bab’ kubwa.
Juzikati kitengo cha Oparesheni Fichua Maovu (OFM) kilichopo chini ya Kampuni ya Global Publishers, kilimfungia kazi mpaka Sinza jijini Dar es Salaam anakoishi, makachero wa OFM wakafanikiwa kukiona mpaka chumba kimoja anachoishi kwenye banda la uani alikopanga.
Kimsingi maisha yake halisi, yako tofauti kabisa na maisha yake ya Instagram. Hana maisha ya kishua kama anavyotaka kuwaaminisha watu, anabangaiza tu kama walalahoi wengine. Siwezi kumhukumu kwa aina ya maisha anayoishi, kwani kwa hali ya sasa, ndiyo maisha yetu! Wengi walianzia kwenye msoto kabla ya kutoboa.

Kim Nana, siyo dhambi kuishi maisha unayoishi! Watu wengi tu wanaishi maisha duni pengine kuliko hata wewe. Hoja yangu hapa, ni kwa nini una-fake maisha yako? Kwa nini umepotoka kwenye ile misingi ambayo awali ulikuwa ukiisimamia na kufuata mkumbo wa waliokutangulia? Acha kufeki na kutafuta kiki mitandaoni, fanya kazi kwani hizo ndizo zitakazokutangaza na ndizo zitakazobadilisha maisha yako.