





Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu- Kanda ya Arusha, Mhe. Mosses Mzuna amewakumbusha Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Ngorongoro kuongeza kasi ya matumizi ya TEHAMA.
Akizungumza na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya hiyo akiwa katika ziara ya kikazi mwishoni mwa wiki iliyopita, Mhe. Jaji Mfawidhi alisema kuwa kipindi hiki cha mabadiliko ya Mahakama ya kutumia TEHAMA watumishi wanalazimika kujifunza na kuelewa matumizi hayo ili kuendana na azma iliyokusudiwa.
Mhe. Jaji Mzuna alitoa mfano juu ya Mfumo wa kusajili mashauri wa Kieletroniki ujulikanao kama JSDS II kuwa ni muhimu watumishi wote kuufahamu ili waweze kwenda sawa na kasi ya mabadiliko hayo.
Mbali na matumizi ya TEHAMA; Mhe. Jaji Mfawidhi aliongeza kwa kuwaasa Watumishi hao kufanya kazi kwa umoja na bidii ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma iliyo bora zaidi.
“Msijihusishe na vitendo vya rushwa kwani vinaharibu Taasisi na pia vitawaharibia maisha yenu, mnachotakiwa kuzingatia ni maadili ya kazi kwa muda wote muwapo eneo la kazi na kutumia lugha nzuri pindi mnapohudumia wateja,” alisisitiza Mhe. Jaji Mzuna.
Katika ziara hiyo alipata taarifa ya kiutendaji wa Mahakama hizo kutoka kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Mhe. Demetrio Nyakunga.
Aidha; Mhe. Jaji Mzuna alipata nafasi ya kutembelea Mahakama ya Mwanzo Waso Loliondo, Mahakama ya Wilaya Longido, Mahakama ya Mwanzo Namanga na kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo jipya la Mahakama ya wilaya ya Longido.
Katika ziara yake, Mhe. Jaji Mfawidhi aliambatana na Watendaji wengine wa Mahakama Kanda ya Arusha, lengo likiwa ni kujitambulisha kwa watumishi na kujua mazingira ya Mahakama zote zilizopo ndani ya kanda ya Arusha.
Na Catherine Francis, Mahakama Kuu Arusha
