
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amemuelezea Rais wa awamu ya tatu Hayati Benjamin William Mkapa kuwa alikuwa na uthubutu wa kulishawishi Taifa kufanya kazi pamoja na Sekta binafsi.
Rais Samia ameyasema hayo leo Julai 14, 2022 katika Kongamano la Kumuenzi Hayati Benjamin Mkapa liliofanyika Visiwani Zanzibar.
Katika Hotuba yake Rais Samia amenukuliwa akisema:
“Alihubiri sana juu ya hili na pia aliutangulia wakati kwa sababu wakati ule bado nchi yetu ina Imani ya kijamaa isiyoamini kushirikiana na Private Sector lakini yeye alikuwa na uthubutu wa kutushawishi kufanya kazi na Private Sector.”
Aidha Rais Samia amesema Hayati Mkapa alikuwa kiongozi shupavu aliyesimamia mabadiliko hayo ingawa ye mwenyewe alikuwa muumini mzuri wa sera za ujamaa ambao ulikuwa hauamini sana ushirikiano na sekta binafsi.

Rais Samia ametumia hotuba yake pia kunukuu kauli aliyoitoa Hayati Benjamin Mkapa katika Mkutano Mkuu wa Halmashauri ya CCM Agosti 5, 2004 Mkoani Dodoma, ambapo alisema:
“Uongozi shupavu hauogopi kubadili mkakati iwapo ni lazima kufanya hivyo, tukishaamua sera tunahitaji ujasiri wa kutenda na siyo maneno, ukiwepo ubishi uwe wa kasi na ubora wa utendaji na siyo tena ubishi wa sera ambayo tulikwisha iamua.”

Rais Samia amesisitiza watanzania watumie muda kutobishana na sera ambazo tayari zimekwisha amuliwa na badala yake watende kulingana na sera hizo kwa kuongeza kasi na ubora kama ilivyokuwa maono ya Hayati Benjamin Mkapa.