KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera amefunga mjadala wa aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Mzambia, Obrey Chirwa kwa kutamka kuwa ‘achaneni naye, tulieni nawaleteeni bonge la straika’.
Kauli hiyo ameitoa ikiwa siku chache tangu kuwepo kwa taarifa za mshambuliaji huyo kutaka kurejea Yanga katika usajili wa dirisha dogo unalotarajiwa kufunguliwa Novemba 15, mwaka huu.
Kocha huyo anayezungumza Lugha ya Kiswahili kwa lafudhi ya Kilingala, hivi karibuni alitamka kuwa hamuhitaji mshambuliaji huyo kwa kile alichokitaja utovu wa nidhamu.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Zahera alisema hana hofu juu ya kiwango cha mshambuliaji huyo, lakini nidhamu ndiyo sababu akiamini akirejea atawavuruga kwa kuhamasisha migomo kwa wachezaji wenzake pale mishahara inapochelewa.
Zahera alisema, tayari anao washambuliaji wazuri wenye uwezo mkubwa zaidi ya Chirwa wanaotarajiwa kujiunga na Yanga wakati wowote, ambao ameanza kuwashawishi watue Jangwani.
Aliongeza kuwa washambuliaji hao atakaowaleta atawafanyia majaribio kwa lengo la kuwaridhisha viongozi kabla ya kuwapa mkataba kama ilivyokuwa kwa Mkongomani mwenzake, Heritier Makambo.
“Sioni sababu ya kung’ang’ania Chirwa arejee Yanga akiwa tayari ameikimbia timu ikiwa katika kipindi kigumu kutokana na kucheleweshewa mishahara.
“Hivyo, sitaki kumuona Chirwa akirejea Yanga, ninawahakikishia Yanga nitawaletea mshambuliaji mwingine mwenye uwezo zaidi ya huyo, watulie usajili ufunguliwe,” alisema Zahera.
WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam