×

NMB YAICHAPA CRDB ‘BANKERS BASKETBALL LEAGUE’

Mchezaji wa timu ya kikapu ya NMB, Danford Kisinda, akiwatoka nyota wa timu ya CRDB wakati wa pambano hilo.

MICHUANO ya Mabenki kwa Mpira wa Kikapu (Bankers Basketball League – BBL 2018), imeendelea kupamba moto hapa nchini, ambapo juzi Jumamosi kikosi cha Benki ya NMB kiliigaragaza timu ya CRDB kwa jumla ya vikapu 52-42.

NMB chini ya Kocha Mkuu Evarist Mapunda, ilitawala kwa kiasi kikubwa pambano hilo lililofanyika kwenye Viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam, ambapo ilimaliza nusu ya kwanza ya mtifuano huo ikiwa mbele kwa vikapu 26-15.

Katika nusu ya pili katika kujiamini kulikopitiliza kuliwafanya nyota wa NMB kupunguza kasi, ambapo walijikuta wakiimaliza nusu hiyo  kwa kipigo cha vikapu 27-26, ingawa havikutosha kuipa CRDB ushindi wa jumla, hivyo ili NMB kushinda ikaibuka na 52-42.

Akizungumza baada ya mchezo, Mapunda aliwapongeza nyota wake kwa upambanaji uliofanikisha kuibuka na ushindi huo na kwamba wamejipanga kuhakikisha wanautwaa ubingwa wa michuano hiyo inayofanyika kila mwaka.

“Tumetimiza lengo la kuibuka na ushindi katika mechi dhidi ya CRDB, nawapongeza nyota wangu kwa upambanaji na sasa tunaelekea kwenye mazoezi kujiandaa na mechi zijazo kulingana na ratiba, ili kufanikisha lengo kuu la kutwaa ubingwa,” alisema Mapunda.

Katika hatua nyingine, timu ya soka ya NMB pia ilifanikiwa kuigaragaza CRDB mabao 3-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Gymkhana, jambo ambalo limeiweka katika mazingira mazuri ya kunyakua ubingwa wa michuano hiyo.

Stori: Sweetbert Lukonge