
Harmonize.
JANUARI 16, mwaka huu katika ukurasa wa Instagram wa mkongwe wa filamu duniani, Arnold Schwarzenegger aliweka picha aliyopiga akiwa amejifunika blanketi chini ya sanamu yake iliyoonesha enzi hizo akitunisha misuli.
Picha ile ilikuwa na maana kubwa sana kwake. Aliamini zama sasa zimebadilika yaani alikuwa kijana na muda mwingi aliutumia kufanya mazoezi na kutunisha misuli. Leo hii hawezi kutunisha misuli kama zamani kwa sababu umri umekwenda. Si wakati wake tena.
Miaka 68 aliyokuwanayo sasa haimfanyi kuwa Arnold yule aliyekuwa akitunisha misuli kabla ya kujiingiza kwenye filamu kisha siasa. Kote huko ameachia vizazi vingine japo kidogo bado yupo kwenye filamu lakini hafanyi kama zamani.
Ukija katika Muziki wa Bongo Fleva kila mwaka kumekuwa na wasanii wapya, japokuwa wanakutana na changamoto nyingi kutoka kwa wakongwe lakini haziwafanyi kutokukubalika. Huu ni wakati wao!
Katika makala haya inawachambua baadhi ya wasanii hao;
Harmonize
Ni zao kutoka Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) inayosimamiwa na Diamond Platnumz. Alianza kukubalika mwaka jana baada ya kuachia Ngoma ya Aiyola. Kuonesha kuwa huu ni wakati wake, kwa sasa anaendelea kubamba vilivyo na Ngoma ya Bado akiwa ameshirikiana na bosi wake, Diamond.
Ruby.
Ruby
Ni wakati wake! Alianza kwa kushinda Shindano la Serengeti Super Nyota 2014 linaloendeshwa na Clouds FM. Mwaka jana akaibuka na Singo ya Na Yule iliyompatia ofa ya kutengeneza kideo chake bure nchini Kenya. Baada ya hapo akaibuka na singo nyingine ya Nivumilie akiwa ameshirikiana na Baraka Da Prince ambazo zote hizo zinabamba hadi sasa.
Galatone
Ni mmoja wa wanamuziki wanaosikilizwa kila kona kwa sasa kupitia wimbo wake mpya wa Samaki aliotengenezewa na prodyuza mkongwe Bongo, Dunga. Wimbo uliomtoa Galatone ulikuwa ni Sina Mali.
Alice
Amekuwa ni mmoja wa muhimili kutoka Jumba la Kusaka Vipaji (THT) kwa sasa. Anakumbukwa zaidi kwenye shoo aliyoitoa wakati wa hafla fupi iliyoandaliwa na wasanii kumuaga aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete iliyofanyika Mlimani City mwaka jana. Usiku huo alifanya maajabu ya kuuimba Wimbo wa Hiba ulioimbwa na Bitchuka kutoka Bendi ya Mlimani Park Orchestra enzi hizo. Kwa sasa Alice anabamba na Ngoma ya Je Utanipenda.
Pam D.
Pam D
Ni mmoja kati ya wasanii wa kike wanaobamba kwa sasa. Pam D ni zao kutoka Defa-tality Music chini ya Prodyuza Mesen Selekta. Wimbo wake uliomtambulisha ulikuwa ni Nimempata uliokuwa ukipata ‘airtime’ za kutosha nchini Nigeria. Kwa sasa anabamba na Ngoma ya Popolipopo inayofanya poa.
Wapo pia wanamuziki wengine wanaofanya poa ambao huu ni wakati wao kama vile Baraka Da Prince, Attu, Heri Muziki, Chemical, Motra the Future, Mo Music na wengine wengi.