×

ASIA MUSTAFA: BINTI ANAYEISHI BILA FIGO KWA MIAKA 12


  ASIA MUSTAFA
ni msichana anayeishi bila figo kwa miaka 12 sasa na alianza kuugua mwaka 2004 ambapo zilifeli zote mbili, hivyo ikabidi mwaka 2005 apandikizwe figo moja.

Baada ya kupandikizwa figo hiyo alikaa nayo mpaka 2011 ambapo ilifeli tena hivyo kuanzia hapo amekuwa akisafishwa damu kwa kutumia mashine (dialysis) kwa wiki mara tatu mpaka sasa.

Mwanadada huyu mwenye umri wa miaka 31, kutokana na changamoto alizopitia katika maisha yake kuhusiana na kuishi huko bila figo, aliamua kuandika kitabu kinachoelezea maisha yake kinachokwenda kwa jina la ‘NIMEISHI BILA FIGO MIAKA KUMI NA MBILI’ ambacho kitakuwa mtaani rasmi, Novemba 17, mwaka huu.

“Ninaishi bila figo kwa miaka 12 sasa, hivyo nikaona ni vyema niandike kitabu ambacho kitaelezea maisha yangu ikiwa ni njia mojawapo ya kuwapa moyo wenye tatizo la figo ambalo ni janga kwa watu wengi,” alisema Asia.

Asia aliendelea kusema kitabu hicho ambacho amekiandika kwa madhumuni ya kuwapa moyo wagonjwa wa figo na kuwaeleza kuwa kuumwa siyo mwisho wa maisha, kuwaelimisha wanaowauguza wagonjwa wa figo kuhusu chakula anachotakiwa kula mgonjwa, changamoto alizopitia na mengine mengi kitapatikana kwa shilingi 10,000 tu, kwa yeyote anayehitaji amtafute kwa namba zake za simu; 0656 684431.

Kwa habari soma katika gazeti la Ijumaa wiki hii linalotolewa na Global Publishers Ltd.

Na Mwandishi Wetu