×

PILIPILI HAIONJWI

PAAAAAMBEEE shoga unaringia kujua kupika wali wa nazi wakati kuyatumia machicha yake huwezi, haloooo eeeeehhhh! Hebu usinikaushe uzazi miye na umbo lako kama mkate wa boflo!

Shoga mahaba ni asali wala hayahitaji sukari na ukitaka kujua uchungu wa kuachwa angalia makalio ya sufuria yakiwa kwenye jiko la moto, warerereeeee!

 

Leo mwenzenu limenifika hapa! Bado nipo na nyie wazazi ambao kila kitu mnaona sawa tu, maisha mnayachukulia kama mnaishi Ulaya, inahu? Heri karipio la rafiki, kuliko busu la mnafiki shoga!

Utakuta mama mtu mzima ana mtoto mmoja lakini huyo mfanyakazi wa ndani anajua kila kitu ndani ya chumba, anajua hadi nguo za ndani za baba zinakaa sehemu gani, hooovyooo! Hivi mnajua umuhimu wa chumba cha wazazi? Jamaaani!

 

Kweli nimeamini uchafu wa kuku mdomoni wa bata nyuma kwake, heee heeeiyaaaa usinione nacheka shoga inatia aibu kweli, huwa najiuliza mara nyingi hivi kuna wanawake hadi leo hawajui umuhimu wa chumba, hawajui kama mfanyakazi wa ndani siyo wa kujua kila kitu cha chumbani hata kuingia tu!

Utakuta dada wa kazi ndiyo amekuwa akifanya usafi chumba cha wazazi, tena hadi uvunguni, amekuwa akikunja na kupanga nguo za wazazi kwenye makabati, wenyewe wanaona ndiyo uzungu na kwenda na wakati, shuuuutuuuuu!

 

Shoga tung’atane tu sikio, wenzetu wanakwambia ukitaka kujua mwenye kiwanja mwaga mchanga. Chumba siyo sebule, chumba cha wazazi siyo cha kuingiza kila mtu, sijui shosti wako kaja kukutembelea unamuingiza hadi chumbani, mfanyakazi wako anajua hadi akiba ya pesa unapoficha, inahu?

 

Vitu vingine mwanamke kuwa kama umefundwa bwana, siyo kila kitu unajifanya mjuaji na mwisho wa siku huyohuyo dada wa kazi anakujua nje ndani, anajua leo baba na mama wamevaa nguo za ndani za rangi gani, nyingine zimetoboka na mbaya zaidi huyohuyo dada wa kazi anajua hadi harufu ya nguo hizo, haloooooo eeeeehhh tena ya kisoda shoga ya bia ntalewa miye!

 

Siyo kila kitu cha kujaribu na kuiga shoga, ndiyo maana hata pilipili haionjwi wala kujaribiwa! Usimfanye dada wa kazi kama sehemu ya majaribio chumbani kwako, afanye kila kitu anachokiona!

 

Mwanamke lazima ujue thamani yako na ya mwenzako, kuna vitu vya kufanya dada wa kazi ajue lakini siyo ajue siri zenu za ndani, kuna wengine wanaweka vitu vya ajabu huko chumbani akijua huyo dada wa kazi itakuwaje?

 

Au basi huyo dada wa watu hujui maisha yake huko alipotoka, siku mbili tatu anakuwekea vitu vya ajabu kitandani kwako mara kamchukua mumeo unaanza kulia, hooooovyooo!

Shoga huwa napata hasira miye kwa mambo kama haya, haya tukutane siku nyingine maana nimeshalitapika lililokuwa limenikwama.

Ni mimi Shangingi Mstaafu Anti Naa wa Ukwee!

SHANGINGI MSTAAFU | Mawasiliano: 0713-761 135