×

SABABU ZA MASTAA KUANIKA MAUNGO YAO

SIKU za hivi karibuni mastaa wengi wa kike wamekuwa wakionekana kupenda kuacha wazi sehemu kubwa ya miili yao. Jambo hili limeifanya jamii kuwadharau na kuwaona hawafai kuigwa kwani wanavyovifanya haviendani na maadili ya Kitanzania.  Serikali nayo imekuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na wale mastaa wanaoachia picha zisizokuwa na maadili mitandaoni zikiwemo zile za nusu utupu.

Uchunguzi wa Risasi Mchanganyiko umebaini mambo mbalimbali yanayosababisha mastaa hao hasa wa kike kupenda kukaa nusu utupu na kujianika kwenye mitandao ya kijamii kama ifuatavyo;

ULIMBUKENI

Mastaa wengi wa kike wanaonekana kuwa na ulimbukeni. Wanaona kukaa nusu utupu ndiyo watakuwa maarufu au kutambulika na kuwa wa tofauti katika jamii.

UZUNGU MWINGI

Licha ya kwamba wao ni Waafrika, lakini wanataka kuwa Wazungu, yaani wanakuwa na mambo ya kizungu zaidi na kuyaendekeza wakidhani ndiyo ustaa wenyewe. Mastaa hawa wamekuwa wakiiga mitindo mbalimbali ya maisha kutoka nje ya nchi kwa kile wanachosema ni kwenda sawa na utandawazi, jambo ambalo wamejikuta wakiharibu kabisa maadili ya Kitanzania kwani hakuna utamaduni huo.

 

Wasanii wengi hawajielewi, hawana elimu ya kutosha kuhusu kile wanachokifanya hivyo elimu yao ni ndogo, hali inayowafanya wahisi kwamba kile wanachokifanya kiko sawa. Hawajui kwamba wao ni kioo cha jamii na wanatazamwa ili kuwa mfano kwa vizazi na vizazi, wao wanaangalia maisha yao ya leo, hawafikirii kuhusu kesho.

 

KUJIUZA/ KUJINADI

Licha ya kwamba wamekuwa wakikana kwamba hawajiuzi, uchunguzi unaonesha kuwa mastaa wengi wa kike wanajiachia nusu utupu mitandaoni ili wapate wanaume ambao watawawezesha kuendesha maisha yao.

Ndiyo maana unakuta msanii ameonekana kwenye filamu moja au video ya wimbo mmoja, lakini maisha yake ni mazuri, ana gari la kutembelea, amepanga nyumba nzuri na mengine mengi, akiulizwa anadai anafanya biashara zake, akiulizwa biashara gani anakuwa na kigugumizi.

MWANASAIKOLOJIA ATOA NENO

Kutokana na kushamiri kwa tabia za mastaa wa kike kukaa nusu utupu, mwanasaikolojia maarufu Bongo ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Chris Mauki alitoa neno hili:

 

“Ukichunguza siyo wanawake wengi, bali ni aina ya wasichana walio kwenye tasnia f’lani na wana kivuli cha umaarufu hususan mitandaoni na bahati mbaya wengi hawajafundishwa kuwa vioo na inamaanisha nini kuwa kioo, ingawa jamii inawategemea kuwa kioo. Huwezi kutegemewa kuwa mwanajeshi na hujasaidiwa kujua uanajeshi ni nini na mtu anakuwaje mwanajeshi.

“Vilevile wengi pia hawajafundishwa kusimama kwenye umaarufu ndiyo maana tabia zao ni shida. “Jambo lingine ni malezi, wengi ukichunguza wana shida ya malezi sehemu fulani kwenye maisha yao, kukosekana kwa malezi thabiti ni uharibifu mkubwa sana kwenye msingi wa watu hawa, ndiyo maana hata mtu aombe radhi au aitwe Polisi huwa mambo yanaendelea tu,” alisema Mauki.