×

MKE WA AZORY AFANYIWA KITU MBAYA! – VIDEO

PWANI: Wakati akitimiza mwaka mmoja tangu mumewe adaiwe kutekwa na watu wasiojulikana, mke wa aliyekuwa mwandishi wa habari wa kujitegemea wa Kampuni ya Mwananchi Communications, Azory Gwanda, Anna Pinoni amefanyiwa umafia.  

 

Wakati Anna akiendelea kuugulia maumivu ya kutekwa kwa mumewe huyo, watu wasiojulikana wamevamia ofisi yake anayofanyia shughuli za ushonaji na kumuibia vitu kadhaa hivyo kuzidi kumpa wakati mgumu.

 

Katika mahojiano maalum na Gazeti la Risasi Jumamosi lilipomtembelea nyumbani kwake, Kibiti mkoani Pwani, mke wa Azory alisema watu wasiojulikana walikosa huruma kwake ambapo Oktoba 11, mwaka huu walimuongezea maumivu kwa kuvunja ofisi yake ya ushonaji ambayo ndiyo inayomfanya ajikimu katika kipindi kigumu alichonacho na kumuibia vitu vilivyokuwemo.

 

Anna alisema katika tukio hilo watu hao walimuibia vitu mbalimbali vikiwemo mashine ya kudarizi, vitenge alivyokuwa akiuza, khanga, nguo za wateja na vitu vingine ambavyo thamani yake ni zaidi ya shilingi milioni moja.

 

“Nikiwa kwenye machungu ya kumsaka mume wangu, Oktoba 11, mwaka huu nilipata pigo lingine la kuvunjiwa ofisi yangu ninayofanyia shughuli za ushonaji ambayo ndiyo ilikuwa nguzo yangu pekee ya kujikimu kimaisha. Ukweli roho imeniuma sana kwa kitendo nilichofanyiwa, kila nikijifikiria, ninajiuliza kwa nini majanga yanazidi kuniandama?

 

“Maana hata huyu mwanangu wa mwisho, Gladness naye nilimzaa kwa shida kutokana kupandwa na presha mara kwa mara kwa sababu ya tukio la kutekwa mume wangu, lakini nilimshukuru Mungu kwa kujifungua salama. “Baada ya kunivunjia ofisi yangu, wasamaria wema waliofahamu juu ya tukio hilo walinipigia simu usiku huohuo.

 

“Nilikimbia haraka kwenda kujionea unyama niliofanyiwa ambapo baada ya kujionea tukio hilo nilikimbilia Kituo cha Polisi cha Kibiti kutoa taarifa. “Pale Polisi nilifungua kesi ya kuvunjiwa na kuibiwa katika jalada lenye namba KBT/ RB/1322/2018,” alisema mke wa Anzory.

 

Mwanamke huyo alisema tukio hilo limemzidishia hofu katika maisha yake na wanawe kwa kuwa anahisi huenda watu wabaya wakawa bado wanaifuatilia familia yake na kudai huenda katika uvamizi huo wangemkuta, wangemuondoa uhai wake au kumfanyia jambo baya zaidi.

 

“Namshukuru Mungu wakati ofisi yangu inavunjwa sikuwepo maana kuna wengine huwa wanalala kwenye ofisi zao kwa ajili ya kulinda, sasa kama nami ningekuwa nafanya hivyo wangenikuta, pengine wangeniua.

 

“Bado nahisi kuna jambo linaendelea juu ya familia yangu na hao watu wasiojulikana,” alimalizia mke huyo wa Azory na kusisitiza kuwa bado Polisi wanaendelea kuwasaka waliomfanyia tukio hilo bila mafanikio.

ITAKULIZA! Mke wa AZORY Apata PIGO Lingine, Asimulia kwa Uchungu!