×

NBC SASA KUHUDUMIA WATEJA WAKE KIDIJITALI MWANZO MWISHO – VIDEO

Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi, akizungumza jambo katika hafla fupi ya kujitambulisha kwa wahariri wa habari za biashara na wateja wa benki hiyo leo jijini Dar es Salaam.
…Akijibu maswali ya wahariri na mameneja mbalimbali wa makampuni.
Mkurugenzi wa Fedha wa NBC, Waziri Barnabas, akifafanua jambo wakati wa mkutano huo kuhusu benki hiyo ilivyojipanga kuongeza wigo wa wateja wao.
Sabi akielezea malengo ya benki yake kwa wateja katika kuwahudumia vizuri zaidi.
Meneja wa Kampuni ya Global Group, Abdallah Mrisho akiuliza swali kuhusu benki hiyo ilivyojipanga hasa kujitangaza kupitia mitandao ya kijamii na namna wanavyotoa huduma zao za kuwasomesha wanafunzi nje ya nchi.
Baadhi ya viongozi wa NBC waliohudhuria hafla hiyo.
Sehemu ya viongozi NBC.
Wageni na waalikwa wakifuatilia kilichokuwa kikiendelea ukumbini.

Meza kuu ikifuatilia mchakato huo kwa makini.

Mmoja wa wahariri wa habari za biashara akiuliza swali.
Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi (katikati) akiwa na viongozi wengine wa NBC.

 

 

BENKI ya Biashara nchini (NBC) imesisitiza itaendelea kuboresha zaidi huduma zake kwa wateja kwa kufanya mabadiliko ya kitamaduni katika benki hiyo.

 

Hayo yalisemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji, Theobald Sabi, wakati alipokutana na wahariri wa habari za biashara na uchumi jijini Dar es Salaam.

 

Sabi aliyataja maeneo makuu waliyodhamiria kuyaboresha ni pamoja na malipo, ufunguaji na ufufuaji wa akaunti, chaneli za kidijiti (ATM, Benki Kiganjani na Benki Mtandao) na utatuzi wa malalamiko hasa urejeshaji wa fedha za wateja katika muda mfupi.

 

Kuhusu huduma za malipo alisema wataangalia upya na kwa undani zaidi taratibu zao za malipo ili kupunguza muda wa miamala ya malipo yanayotoka matawini na makao makuu.

 

“Eneo la malipo ni eneo muhimu sana kwa wateja wetu na ndiyo maana tunataka kuimarisha eneo hili lifikie viwango vya kimataifa kwa mantiki ya muda unaochukuliwa kukamilisha miamala ya malipo,” alisema na kusisitiza kuwa benki yake itakuwa karibu zaidi na wateja wake katika matawi yote kwa kukutana nao mara kwa mara  ili kupata mrejesho na huduma na bidhaa zao kutoka kwa wateja.

 

Alisema pia kwamba hivi sasa benki hiyo ina mkakati wa kujenga benki ya kidijiti ambayo itarahisisha maisha kwa wateja wake ambapo hivi sasa wanawekeza kwenye mifumo mipya inayobeba huduma za kidijiti zinazokidhi mahitaji ya wateja kwa kuokoa muda, gharama na usumbufu ambapo wateja watafanya miamala yao popote na wakati wowote.

 

“Kwa mfano, tumerahisisha miamala ya malipo kwa wateja wetu wakubwa kupitia mfumo wa IFEC. Wateja hawa wanaweza kufanya miamala ya malipo bila kuja benki na kujaza makaratasi,” alisisitiza.

 

Hatua nyingi katika kuboresha huduma hizo, ni kukuza hisa katika soko ambapo NBC imedhamiria kukuza mapato yake katika kipindi kijacho kwa kujikita kwenye mifumo mipya, bidhaa  mpya, utoaji wa huduma bora na kuwekeza kwenye huduma za kidijiti katika maeneo makuu matatu ambayo ni: wateja binafsi, wateja wadogo na wa kati na wateja wakubwa.

 

Kuhusu uhusiano wake na serikali, ambayo inamiliki asilimia 30, alisema itawajibika kulinda maslahi ya mwanahisa huyo wa NBC kwani ni moja ya benki chache zinazoaminiwa na serikali kujiunga na Mfumo wa Malipo Serikalini (GePG) ili kukusanya maduhuli ya Serikali.

 

Akizungumzia dhamira ya serikali kuifanya nchi kuwa ya viwanda, Sabi alisema benki hiyo inaunga mkono dhamira hiyo kwa kuwawezesha wafanyabiashara katika sekta mbalimbali  na mitaji ya kifedha.

 

Sabi alivitaja pia vipaumbele kadhaa katika kuboresha huduma hizo ambavyo ni kuongeza idadi ya wateja na kuyafikia maeneo mengine ambako benki hiyo haipo.

 

“Utumiaji wa teknohama kwa kiasi kikubwa utatanzua changamoto nyingi katika kutekeleza miamala mbalimbali ya kibenki pamoja na ya wateja wetu hivyo kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza tija,” alisema  kuhusu kipaumbele cha matumizi zaidi ya teknohama.

 

Kipaumbele kingine, alisema, ni kuwajengea uwezo wafanyabiashara nchini kuendesha biashara zao  kwa kuwasajili kwenye vilabu maalum vya biashara vijulikanavyo kama NBC Business Clubs kwa ushirikiano uliopo na  Mamlaka ya Biashara Tanzania (Tantrade), Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Chama cha Wafanyabiashara wa Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

NBC YAAHIDI KUWAHUDUMIA WATEJA KIDIGITALI