×

Zahera Awaonya Simba Kwa Bomba

Winga Reuben Bomba kutoka DR Congo.

 

KOCHA mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera ametamba kwamba wamelamba dume baada ya kumnasa winga Reuben Bomba kutoka DR Congo huku akitoa tahadhari kwa wapinzani wao kwamba wanatakiwa kujiandaa kisawasawa kumzuia.

Hata hivyo hili linaonekana kuwa dongo kwa Simba ambao ndiyo wapinzani wakubwa wa Yanga kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kwa sasa.

Bomba ambaye ametoka akademi moja na nyota mkubwa ulimwenguni Cristiano Ronaldo yupo hapa Bongo kwa wiki kadhaa akiwa kwenye hatua za mwisho za kumalizana na Yanga inayoongoza ligi ikiwa na pointi 41.

Akizungumza na Championi Jumatano, Zahera amesema kwamba anaujua vizuri uwezo wa Bomba ambaye anaamini kwamba akianza kuitumikia timu hiyo atakuwa amemaliza tatizo la winga ambalo limekuwa likikisumbua sana kikosi chake.

“Nimefanya kazi na Bomba na ninamjua vizuri sana, ninaijua shughuli yake anapokuwa uwanjani, ninaamini kwamba atapoanza kucheza atakuwa msaada mkubwa sana kwetu na niwaambie tu wapinzani wetu kwamba wajiandae kupambana naye.

“Lakini pia yeye (Bomba) atakuwa suluhisho la tatizo la winga ambalo linakisumbua kikosi changu licha ya kwamba nimewapa nafasi wachezaji kadhaa wacheze, kwani yeye ana uwezo mkubwa sana anapocheza katika nafasi hiyo,” alisema Zahera.