SHIRIKISHO la soka nchini Kenya (FKF) limesimamisha shughuli zote rasmi za soka nchini humu baada ya uthibitisho wa tukio la kwanza la kuepo mwathirika wa virusi vya Corona nchini humo.
FKF tayari limesimamisha mashindano yote rasmi ya vijana, mashindano ya wanawake ikiwemo ligi ya wanawake, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili.
Ligi Kuu ya soka nchini humo KPL itaendelea na ratiba yake wikiendi hii kwa mechi kadhaa kupigwa lakini bila ya uwepo wa mashabiki, huku agizo la kusimamisha michezo hiyo likitarajiwa kuanza kutekelezwa kuanzia Jumatatu, Machi 16.
Pia, katika kujihadhari na virusi hivyo, shirikisho limeziagiza klabu zote nchini humo kusitisha shughuli zote zinazohusisha mikusanyiko ya wachezaji, wafanyakazi wa klabu au mashabiki kama programu za mazoezi, mikutano na mikusanyiko ya mashabiki.
