


WAZIRI wa Kilimo, Japhet Hasunga, ameagiza kurejeshwa ndani ya miezi mitatu madeni yote yaliyokopwa kwenye vyama vya akiba na mikopo (SACCOS) akisisitiza wale watakaoshindwa kutii maelekezo hayo katika kukamilisha deni lake ndani ya miezi mitatu hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
“ Nataka kila aliyekopa kwenye Saccos arejeshe deni lake kwa kufuata utaratibu wa makubaliano na kama wasipotekeleza ndani ya miezi mitatu niliyotoa serikali itaagiza wahusika wote kukamatwa maana dawa ya deni ni kulipa,” alisema.
Hasunga aliyasema hayo jana (Ijumaa) wakati wa kikao cha kazi katika ukumbi wa mikutano wa Mkoa wa Mtwara alipokuwa akizungumza na viongozi wakuu wa vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) na Vyama vya Msingi vya Ushirika vilivyopo katika Mkoa wa Mtwara.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Kaimu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini, Mkaguzi wa Vyama vya Ushirika na Saccos, Kaimu Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Mtwara, wenyeviti na watendaji wa SACCOS na vyama vya msingi vya ushirika Mtwara.
Alilitaja Shirika la Ukaguzi wa Hesabu za Vyama vya Ushirika (COASCO) kutimiza majukumu yake kwa weledi kwa kukagua na kuhakikisha vyama vyote vinafunga mahesabu huku akitaka vyama ambavyo sio hai kuchukuliwa hatua.
Pia aliagiza kila chama Tanzania kiwe na daftari la wanachama walio hai na wafu sambamba na kuhakikisha kuwa viongozi wote wawe na maadili na uwezo wa kuvisimamia vyama vyao ipasavyo.
Katika hatua nyingine alimtaka Mrajis wa Ushirika nchini, Tito Haule, kuwasilisha mpango kazi wa namna ya kukutana na wanachama wa ushirika nchi nzima katika kutatua changamoto zao.
“Na ni lazima taarifa itengenezwe ikionyesha idadi ya vyama mlivyokutana navyo na kueleza ni mambo gani mmezungumza kila mwezi,” aliagiza.
Aliongeza kuwa viongozi ni lazima kutoa mapendekezo ya mabadiliko ya Sheria ya Ushirika itakayosaidia kuondoa usumbufu kwenye ushirika ili uendelee kuwa mkombozi wa wananchi.
“Mje na mfumo wa namna ya kuwasaidia wananchi kupata pembejeo bila kuingia madeni yasiyokuwa na tija,” alisisitiza.