
TAMASHA la Tuzo za Sinema Nchini lijulikanalo kama Sinema Zetu International Film Festival (SZIFF) limezinduliwa rasmi usiku wa kuamkia jana Jijini Dar es salaam.
Uzinduzi huo ulifanyika katika ukumbi wa Sinema ulipo jengo la City Mall katikati ya jiji la Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Balozi wa Kenya hapa nchini, Dan Kazungu.
Katika uzinduzi huo, baadhi ya wageni waalikwa walipata nafasi ya kuangalia sinema ya kutoka hapa nchini iitwayo Red Flag ambayo imeigizwa na Mtanzania, Rammy Galis.
Sinema hiyo ndiyo pekee ya kutoka Tanzania ambayo itashindanishwa na nyingine 31 kutoka mataifa mbalimbali.
Rammy Galis amepata shavu hilo kutokana na sinema yake hiyo kudaiwa kukidhi viwango vya kimataifa kutokana na kutumia Lugha ya Kiingereza.
Akizungumza na Spoti Xtra, Mkuu wa uendeshaji wa Azam Media, Yahya Mohammed, alisema kuwa wanajivunia namna tamasha la SZIFF lilivyoamsha ari na hamasa kwa waandaaji na wapenzi wa filamu nchini lakini pia ni moja ya njia kubwa ya kuzitangaza filamu za Tanzania kimataifa kupitia Televisheni.
“Pia katika tamasha hilo tuna mpango wa kualika mabalozi pamoja na waandaaji maarufu wa sinema kutoka mataifa mbalimbali yaliyopiga hatua ili waje kuangalia filamu zao zikitathiminiwa na Watanzania.”