Rais Dkt. John Magufuli leo Jumatano, Januari 23, 2019 amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya Dini, Ikulu Jijini Dar es Salaam ambapo amesema yeye hajazuia mikutano ya kisiasa wala kuminya Demokrasia badala yake wanasiasa hao wanatakiwa kufuata taratibu ili kuepusha uvunjifu wa amani.
Kauli hiyo ya Rais imekuja baada ya Mchungaji Lyimo kumweleza Magufuli kuwa suala la Demokrasia ni muhimu, watu wana hofu hata kama Rais haelezwi na watendaji wake, huku akimsifu kwa kazi anazofanya na kumtaka atoe uhuru ili watu waseme.
“Mikutano ya kisiasa haijazuiwa. Hatujawazuia wabunge kufanya mikutano kwenye majimbo yao. Hata wakitaka kufanya kila siku, kinachozuiliwa ni kutoka Jimbo moja kwenda kutukana Jimbo la mwingine. Hakuna demokrasia isiyo na mipaka.
“Nataka vyama yyetu viige mfano mzuri wa viongozi wa dini wanavyoheshimiana na kupendana, kwa sababu jukumu langu mlinipa ni kuilinda amani ya Tanzania, hakuna mtu aliyezuiliwa kufanya mikutano mahali pake.
“Hakuna anaemzuia Kubenea kufanya mkutano kwenye Jimbo lake la Ubungo, Mbowe kwenda kufanya Mikutano kwenye Jimbo lake la Hai. Hakuna anayekatazwa kufanya mikutano, wanaendelea kufanya na nyinyi ni mashahidi, hakuna mtu aliyezuiliwa kufanya mikutano mahala pake.
“Demokrasia sio maandamano, huwezi kujenga barabara wakati wengine wanaandamana. Ndiyo maana Marekani huwezi kumsikia Bi. Clinton akifanya kampeni, wamemuachia Rais Trump ambaye amepewa dhamana hiyo baada ya kushinda uchaguzi, watampima baada ya miaka minne.
“Nataka vyama vyetu viige mfano mzuri wa viongozi wa dini wanavyoheshimiana na kupendana, kwa sababu jukumu langu mlinipa ni kuilinda amani ya Tanzania, hakuna mtu aliyezuiliwa kufanya mikutano mahali pake,” amesema Rais Magufuli.
