
DAR ES SALAAM: Kwani anateseka? Kufuatia tetesi za mitandaoni kuwa mzazi mwenza wa mwanamuziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ yupo kwenye ‘stresi’ ile mbaya kutokana na upweke kiasi cha kuamua kupiga ulabu kupitiliza, daktari amemuonya mwanamama huyo juu ya ishu hiyo.
Kwa mujibu wa kurasa za ubuyu za mitandao ya kijamii, Zari ambaye Februari 14, mwaka huu atatimiza mwaka mmoja tangu alipotengana na Diamond au Mondi, amekuwa ni mtu mwenye msongo huku ‘akiwajibu ovyo’ watu wanaoweka maoni kwenye picha zake katika ukurasa wake wa Mtandao wa Instagram.
MFANO WATOLEWA
Ulitolewa mfano kwamba, hivi karibuni kuna mtu alimuuliza; “Hivi Zari huna mpango wa kumtafuta mume mwingine wa kuzeeka naye? Ambapo katika majibu yake, Zari aliwaka; “Mume wangu siyo wa Social Media (Mitandao ya Kijamii), ni mume wangu siyo wetu.” Ilidaiwa kuwa, majibu hayo yaliashiria ‘hayupo vizuri’ na kwamba hakupendezwa na swali hilo kwani kama hakuwa ‘amemaindi’, basi angemjibu kistaarabu.
HARUDI KWENYE UBORA
Mitandao hiyo ilieleza kuwa, Zari hajawahi kurudi kwenye ubora wake na kuwa na amani rohoni tangu alipoachana na Diamond. “Zari anaonekana ana stresi za kufa mtu na sasa hivi ameamua kujipoza kwa mvinyo mkali,” ilisomeka sehemu ya stori hizo za mitandaoni.
AKIRI KUWA KWENYE STRESI
Hata hivyo, katika mitandao hiyohiyo, Zari alikiri kuwa kwenye stresi kwa mwaka 2018 kutokana na kuvunjika kwa penzi lake na Mondi au Baba T, lakini akaahidi mwaka huu atakuwa mtu mwingine kwani hataki kukutana na stresi za aina hiyo tena.
DAKTARI AMUONYA
Kufuatia hali hiyo, mmoja wa madaktari maarufu jijini Dar, Dk Godfrey Chale alilieleza Amani juu ya madhara yanayoweza kumpata Zari endapo ataendelea kuwa kwenye hali hiyo bila kuamua kupatiwa tiba itakayomsahaulisha na kusonga mbele. “Msongo wa mawazo unajulikana kama sehemu ya maisha ya kawaida. Mwili unaweza kuitikia hali hii kiakili na kimwili. “Hata hivyo, kama kweli Zari ana msongo wa mawazo, unaweza kumsababishia athari mbaya kama zifuatavyo;
KUKOSA USINGIZI
“Kwanza msongo wa mawazo unaweza kumharibia mzunguko wa usingizi. “Hali hiyo inaweza kuathiri vibaya ubora wa usingizi na kusababisha kukosekana kwa usingizi. Kama tunavyojua usingizi ni sehemu muhimu ili kuhakikisha afya inakuwa nzuri. Kukosa usingizi huko kunaweza kusababisha madhara hasi kwa afya ya akili na kimwili kwa binadamu. “Ukiona mtu anakosa usingizi kwa sababu ya msongo, mtu huyo anapaswa kumuona daktari haraka iwezekanavyo,” alisema daktari huyo na kuendelea:
KUVURUGA MFUMO WA CHAKULA
“Msongo pia unaweza kuvuruga mfumo wa chakula mwilini. Huvuruga homoni, kupumua haraka na moyo kwenda kasi. Huvuruga pia mfumo wa chakula na kusababisha tumbo kujaa gesi, husababisha maumivu ya tumbo, kutapika na kichefuchefu.

KUPUNGUZA KINGA
“Msongo hupunguza kinga za mwili. Unapokuwa na msongo, kiwango cha homoni ya cortisol katika mwili huongezeka na kinaweza kubadilisha mfumo wa kinga. “Msongo huathiri vibaya kinga ya mwili hivyo kumuweka mtu kwenye hatari kubwa ya maambukizi, baridi na homa. Pia huongeza nafasi ya kuwa na magonjwa mengine kama kisukari na ugonjwa wa moyo.
ATHARI KWENYE UBONGO
“Pia msongo unaweza kuwa na athari kwenye tishu za ubongo. Sote tunajua kwamba stresi zinaleta athari mbaya katika ubongo ambayo ni moja ya madhara ya juu ya afya ya binadamu. “Mbali na madhara mengine ya msongo wa pia unaweza kusababisha kuzeeka mapema.
SHINIKIZO LA DAMU
“Lakini kubwa zaidi, msongo humweka mtu kwenye hatari kubwa ya maumivu ya kifua, shinikizo la damu, mapigo ya moyo kwenda haraka au ugonjwa wa moyo. “Kutokana na madhara hayo ndiyo maana kitaalam ninapendekeza Zari apunguze mawazo na kukubali kwamba jambo lilishatokea na kuamua kusonga mbele akishindwa atafute wataalamu wa afya wamsaidie.”
ZARI NA MONDI
Pamoja na kutengana huku Mondi akidaiwa kunasa kifaa kingine ambacho ni mrembo kutoka Kenya, Tanasha Donna, Zari yeye bado hajamweka hadharani mpenzi mpya. Hata hivyo, kumekuwa na shinikizo la mashabiki wakitaka Mondi kumwangukia Zari ili warudiane kwani kwa mtazamo wao ndiye anayemfaa katika maisha.
ZARI NA GLASI ZA MVINYO
Katika siku za hivi karibuni kupitia mitandao ya kijamii ilisambaa picha inayomuonesha Zari akiwa amekaa kitandani huku ameshikilia glasi inayoonekana kuwa na kinywaji. Wengi kati ya walioiona walisema mrembo huyo alionekana kuwa amelewa akidaiwa alikuwa anasumbuliwa na upweke.
“Hata mimi siwezi kulala peke yangu kwenye kitanda kikubwa kama hicho lazima usingizi utakata ndiyo maana mama kaamua kujipigilia maji ili apate chaji ya kulalia,” ilisomeka moja kati ya komenti iliyowekwa mitandaoni ikiambatanishwa na picha hiyo ya Zari ambayo imetumika ukurasa wa mbele wa gazeti hili.
