×

Jembe Jipya Simba ni Kiwembe Afrika

SIMBA wapo kwenye mchakato wa kumsajili mshambuliaji Mtogo, Hunlede Kissimbo lakini rekodi zinaonyesha kwamba straika huyo ana uzoefu mkubwa wa michuano ya kimataifa ambapo ameshiriki mara kadhaa na Klabu yake ya AS Togo Port de Lomé. Mbali ya straika huyo pia Simba wameshusha beki wa kati kutoka nchini Ghana, Moro Lamine akitokea Buildcon FC Zambia.

 

Kissimbo alitua jijini Dar hivi karibuni ikiwa ni siku chache baada ya Simba kupokea kipigo cha mabao 5-0 kutoka kwa AS Vita kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wakiwa nchini DR Congo. Mshambuliaji huyo ametua nchini akiwa sambamba na mchezaji mwingine wa Ghana ambapo walianza kazi mbele ya Kocha wa Simba, Patrick Aussems raia wa Ubelgiji, juzi Jumatatu katika Uwanja wa Boko Veterani, Dar.

 

Staa huyo ameletwa maalum kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji la Simba linalochezwa na Emmanuel Okwi, Meddie Kagere na John Bocco. Rekodi zinaonyesha kwamba straika huyo msimu uliopita akiwa na timu yake AS Togo Port de Lomé, aliingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo alifunga mabao mawili.

 

Katika kundi hilo, Mtogo huyo walipangiwa na timu za Mamelodi Sundowns, Wydad Casablanca na Horoya ambapo alifunga bao moja dhidi ya Mamelodi Sundowns huku bao lingine akifunga kwenye mechi za hatua ya awali.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescensius Magori alisema: “Wachezaji hao wamekuja kwa mapendekezo ya kocha ambaye atawaangalia kabla ya kufanya maamuzi kwa kuwa tunataka kufanya maboresho kwenye michuano ya Caf lakini watatumika kwenye michuano ya SportPesa.” Waandishi Ibrahim Mussa, Said Ally, Martha Mboma na Musa Mateja.