RAIS John Magufuli amewataka wakuu wa wilaya na viongozi wengine nchini kutotumia mamlaka yao vibaya kwa kuwaweka ndani baadhi ya watendaji wenzao kinyume na sheria.
Magufuli amesema hayo leo Jumanne, Januari 29, 2019 wakati akihutubia baada ya kuwaapisha majaji, wakuu wa wilaya na wakurugenzi ambao aliwateua juzi (Jumapili) ambapo alibainisha sababu za kuwatengua waliokuwa kwenye nafasi hizo kuwa ni kutokana na kutumia vibaya mamlaka yao.
“Ninafahamu sheria za kuweka watu ndani mnazo, lakini msizitumie vibaya, mtu anawekwa ndani halafu baadaye mnamtoa eti amejifunza, bila kumpeleka Mahakamani, ” alisema rais akisisitiza kwamba hilo si jambo jema.
Aliwataka wakuu wa wilaya kuyatumia vizuri mamlaka yao ili kuwepa malalamiko. Pamoja na agizo lake hilo aliwataka pia viongozi hao wajirekebishe na kushirikiana ili waweze kuwasaidia wananchi katika kutatua shida zao.