
BUKOBA: MWISHO wa enzi! Safari ya maisha ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba imetimia juzi baada ya kulazwa kwenye nyumba yake ya milele.
Maelfu ya wananchi na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Bregedia Jenerali Marco Gaguti walifurika tangu juzi Jumapili, nyumbani kwa Ruge ambaye ni mtoto wa Profesa Mutahaba, katika Kijiji cha Kabale, Tarafa ya Kiamutwara, Kata ya Karabagaine, Bukoba mkoani Kagera.

MAZISHI YAWEKA REKODI
Lengo la umati huo lilikuwa ni moja tu, kumpumzisha Ruge ambaye jina lake kwa kirefu ni Rugemarila, waliyemtaja kuwa shujaa wao na kuweka rekodi ya kuwa mazishi yaliyohudhuriwa na watu wengi zaidi mkoani hapa.
Mafuriko yalianza mapema juzi Jumapili, kwenye Uwanja wa Ndege wa Bukoba ambapo watu wengi walikusanyika kushiriki mapokezi ya mwili wa Ruge aliyefariki dunia wiki iliyopita, Februari 26, mwaka huu nchini Afrika Kusini alipokuwa amelazwa kwa matibabu ya figo.
Mara baada ya mwili huo uliobebwa na Ndege ya ATCL kuwasili uwanjani hapo, magari mawili yaliongoza msafara kuelekea kijijini Kabale ambapo ‘plate number’ zake zilikuwa na maandishi ya R.I.P Ruge. Pia magari mengine katika msafara huo yalitolewa namba na kuandikwa neno ‘msiba’ huku njiani kukiwa na vibao vilivyokuwa vikielekeza eneo la msiba kijijini Kabale.
VILIO KILA KONA
Baada ya mapokezi, msafara ulipita mitaa mbalimbali mjini Bukoba ili kutoa nafasi kwa watu kuulaki ambapo vilio vilitawala kila kona msafara huo ulipokatiza. Baada ya hapo msafara huo ulielekea Kabale ambapo jana asubuhi uliagwa kwenye Viwanja vya Gymkhana katika Halmashauri ya Bukoba na mazishi ya kihistoria kufanyika baadaye jioni.
Msafara huo ulipita katika maeneo ya Kituo cha Mabasi cha Bukoba, Hamugembe Rwamishenye kisha kuelekea Kijiji cha Kabale. Watu wengi walijipanga barabarani ulipokuwa ukipita msafara huo ambapo Bukoba ilizizima na kuloa kwa machozi ya waombolezaji ambao walikuwa hawaamini macho yao kuwa mtu wao kipenzi alikuwa amerejeshwa nyumbani akiwa amelala kwenye jeneza.
UFINYU WA NAFASI
Kutokana na ufinyu wa nafasi na wingi wa watu nyumbani kwao na Ruge, mkuu wa mkoa huyo Bregedia Gaguti, alisema waliliona hilo mapema na kulazimika kuhamishia zoezi hilo Viwanja vya Gymkhana ambapo baada ya zoezi la kuaga mwili huo ulipelekwa Kabale kwa ajili ya ibada na mazishi kwenye makaburi ya familia ya Mutahaba.
WENGI WAPOTEZA FAHAMU
Kufuatia zoezi hilo la kuaga, waombolezaji wengi walipoteza fahamu kutokana na kutoamini kama mtu aliyekuwa na mchango mkubwa kijijini hapo alikuwa ameondoka. Bregedia Gaguti alisema kuwa, wingi wa watu ulitokana na namna Ruge alivyoyagusa maisha yake na kwamba walitaka kumuenzi na kumuaga mtu huyo mzalendo na mwanaharakati wa kweli.

RUGE NI NANI?
Anaitwa Rugemarila Mutahaba ambaye alizaliwa Mei Mosi, 1970 huko Brooklyn, New York nchini Marekani. Alikuwa mtoto wa kwanza kwa Profesa Gelase Mutahaba na Christina Mutahaba. Amefariki akiwa na umri wa miaka 49.
ELIMU
Ruge alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi ya Arusha, kuanzia darasa la kwanza hadi la sita kisha akahamia Shule ya Msingi Mlimani jijini Dar ambako alihitimu elimu ya msingi.
Baadaye alijiunga na Shule ya Sekondari ya Forodhani na kuhitimu kidato cha nne kisha kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari ya Pugu ya jijini Dar es Salaam. Ruge alihitimu Shahada ya Masoko kisha Shahada ya Sanaa katika Uchumi kwenye Chuo Kikuu cha San Jose huko California, Marekani.
TAALUMA
Baada ya masomo, Ruge aliporejea Tanzania kutoka Chuo Kikuu cha San Jose ambako alihitimu masomo yake, alianza kutambulika kwenye jamii baada ya kuanza kufanya kazi na rafiki yake, Joseph Kusaga ambaye alikuwa akiendesha klabu ya usiku ya disko iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Clouds Disco.
Ushirikiano wao ulisababisha kuanzishwa kwa Clouds Media Group jijini Arusha ambapo licha ya kuwa chombo cha habari na burudani kwa hadhira, hasa vijana, ilifanya kazi ya kuhamasisha vijana wadogo wa Kitanzania kujiingiza katika kutafuta fursa na ujasiriamali ili kujiinua na kuchangia katika maendeleo ya jamii zao na taifa kwa jumla.

Tangu maisha ya utotoni, Ruge alikuwa mpenda muziki, lakini kipaji chake hakikuwa kwenye muziki peke yake. Alikuwa mchezaji mpira wa miguu (soka) na alipewa majina mengi kwa kipaji hicho akicheza timu za mtaani za Chuo Kikuu kuanzia Adanco na Summer Rangers na alifikia hatua ya kuchaguliwa katika Timu ya Mkoa wa Dar ya UMISETA (Umoja wa Michezo Shule za Sekondari Tanzania).
Pia Ruge alikuwa na kipaji cha kuandika. Vipaji vyake vyote havikuweza kunawiri kwani alikuwa na mapenzi na muziki zaidi, hivyo kustawi zaidi katika eneo hilo.
FAMILIA
Ruge alikuwa mtoto wa kwanza kati ya watoto watano kwa Profesa Mutahaba na Christina Mutahaba, hakuwahi kufunga ndoa, lakini ameacha watoto watano.
MARADHI NA KIFO
Ruge alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya figo hivyo alipelekwa Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu hadi mauti yalipomfika Februari 26, 2019. Watanzania wengi waliopokea habari za kifo chake, wakiwa ni pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli, walionyesha kushtushwa.
Hiyo ni kutokana na mchango mkubwa wa Ruge katika tasnia ya habari na burudani, ubunifu katika mipango mikakati, kuendeleza vipaji vya vijana wa Kitanzania, kuhamasisha ari ya ufanyaji kazi kwa bidii katika jamii na maendeleo ya Tanzania kwa jumla.
KUTOKA KWA MHARIRI
Tunawapa pole familia nzima ya Profesa Mutahaba kwa msiba huu mzito uliowakuta, familia ya Clouds Media Group na tasnia ya sanaa na burundani nchini.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa, Jina lake lihimidiwe – Amina.