
WALAINI TU! Ndivyo unaweza kusema baada ya kila kiongozi, mchezaji na hata kocha wa Simba kusema wamekwenda Algeria kushinda tu. Kuonyesha hilo linawezekana Simba walipotua tu kwenye ardhi ya Algeria wala hawakutaka kwenda moja kwa moja Bechar ambako mechi yao na JS Saoura inapigwa leo na badala yake walibaki mjini Algiers.
Simba ambayo leo itapambana na wenyeji wao, Saoura kwenye Uwanja wa 20 Aout 1955 unaoingiza mashabiki 15,000 uliopo mjini Bechar, walitua Algeria tangu Alhamisi jioni na kuweka mapumziko mafupi mjini Algiers kabla ya jana, majira ya saa tano na nusu asubuhi kwenda Mji wa Bechar ambako ndiko mechi itapigwa.
Mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika inatarajiwa kupigwa majira ya saa 4:00 Usiku kwa saa za Tanzania ambapo Watanzania wengi watakesha kusubiri mtanange huo. Mechi ya kwanza iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar Simba ilishinda mabao 3-0.

Crecentius Magori ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Simba, aliliambia Championi Jumamosi kuwa, walizifahamu mapema figisu za wapinzani wao, ndiyo maana waliamua kuweka kambi kwenye mji
jirani wa Algiers.
Magori ambaye ndiye kiongozi msomi zaidi kwenye klabu za Ligi Kuu Bara, aliongeza kuwa, kikosi chote kipo fiti na hakuna majeruhi na wamefanya mazoezi ya siku mbili na waliamua kufanya mazoezi ya mwisho jana usiku kwa lengo la kuwavuruga wapinzani wao.

“Tutatoka leo (jana) saa tano asubuhi, tutafanya mapumziko mafupi pale Bechar, kisha jioni tutaenda kwenye Uwanja wa Aout 1955 ambao tutachezea mechi yetu, kwa ajili ya mazoezi ya mwisho.
“Kwa upande wa wachezaji na benchi la ufundi washamaliza kazi yao, ambapo mwalimu amenihakikishia kuwa tutafanya vizuri kwenye mchezo huu, kutokana na maandalizi na saikolojia ya wachezaji kuwa vizuri,” alimaliza Magori.
MBELGIJI: HATUTARUDIA MAKOSA
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems raia wa Ubelgiji ameweka
wazi kwamba hatakubali kurudia makosa yaliyotokea kwenye michezo miwili iliyopita ya ugenini walipocheza na AS Vita ya Kinshasa Congo na ule wa Al Ahly ambayo yote walifungwa mabao 5-0.
“Hatutakubali kufanya makosa kwa mara ya tatu mfululizo ya kukubali tunafungwa tena idadi kubwa ya mabao kama tulivyocheza na Al Ahly na AS Vita katika michezo iliyopita ya ugenini.
“Nataka kuona katika mechi hii tunashinda kwa mara ya kwanza
ugenini baada ya kufungwa mara mbili mfululizo, tayari nimewaambia wachezaji hivyo nina mategemeo makubwa ya kupata ushindi katika mchezo huu.
“Ninaamini mchezo utakuwa mgumu Saoura wako nyumbani lazima watataka matokeo mazuri, lakini tumejiandaa kuhakikisha tunafanya vizuri na hatutarudia makosa ya michezo ya nyuma iliyopita hayo ndiyo malengo yetu,” alisema Aussems.
“Katika mchezo huu nitamkosa Okwi ambaye tayari nilishawaandaa wabadala wake ambao ni Dilunga (Hassani) na Juma (Rashidi) na Juuko ambaye yeye nafasi itachezwa na Bukaba (Paul) ambaye naye nilianza kumuandaa tangu michezo miwili iliyopita ya ligi kwa kumpanga na Wawa (Segre) katika kuhakikisha wanazoeana kwa haraka,”aliongeza Kocha huyo.
Kikosi cha Simba kitakachoivaa Saoura kinatarajiwa kuwa hivi; Aishi Manula, Zana Coulibaly, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Bukaba, Wawa, James Kotei, Clatous Chama, Jonas Mkude, Meddie Kagere, John Bocco.
WAARABU WAPAGAWA
Kuonyesha kuwa wameanza kuingia mchecheto, uongozi wa JS Saoura kupitia kurugenzi ya ufundi inayoongozwa na Hossein Abdul Wahab, juzi walinasa video za mwisho za mechi za Simba za Ligi Kuu Bara na kujifungia kuona namna ya kuwakabili.
Katika taarifa iliyotumwa kwenye mtandao wa timu hiyo, zinasema kuwa wamefanikiwa kunasa baadhi ya mikanda ya mechi za Simba ambapo wametumia muda mwingi na wachezaji kuweza kuangalia mbinu za madhaifu yao kabla ya mchezo wao wa leo Jumamosi.Taarifa ya Wahid inaendelea kusemwa katika mechi hizo walizoangalia na wachezaji wameweza kubaini mambo mengi hivyo wanaimani kubwa ya kuweza kufikia malengo yao katika mchezo huo muhimu kwao.
“Ndoto yetu ni kuona tunafanikiwa kufuzu robo fainali, tunajua wapinzani wetu ni imara lakini haiwezi kukatisha ndoto yetu katika michuano hii ikiwa ni mara ya kwanza kwetu,” ilisema
taarifa ya kwenye mtandao wao.
Imeandikwa na Issa Liponda, Wilbert Molandi na Ibrahim Mussa