
KAMPUNI za Bakhresa ambayo inazalisha vyakula na vinywaji, imerudisha kinywaji cha Vimto baada ya kuingia ubia na kampuni ya Nichols Plc.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa kampuni hizo, Said Salim Bakhresa, alisema kuwa wamefurahi kukileta kinywaji laini cha Vimto nchini Tanzania na kutangaza ubia wao mpya na Nichols.
“Tumefurahi sana kuingia ubia na Nichols na kurudisha nyumbani kinywaji cha Vimto ambacho kilipotea kwa muda mrefu. Nakumbuka nilikuwa mdogo kipindi hicho, kwa hiyo kinarudi na kitapatikana katika maduka yote,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Nichols Plc, Kanda ya Afrika, Robert Hammersley, alisema kuwa wamefurahi kuungana na Bakhresa na kuzindua kinywaji hicho kwa sasa na wanatarajia kufanya naye kazi nyingi.
“Tunatarajia kufanya kazi na Bakhresa kwa sababu ni mbobezi katika sekta ya viwanda Afrika Mashariki, na Tanzania ni soko muhimu la kimkakati kwetu na mahali ambapo Vimto ina historia Vimto iliwahi kuwepo miaka ya nyuma na sasa tumepata sehemu ambayo tunaweza kuirudisha tena ikazalishwa na kusambazwa kwa Watanzania. Tutaendelea kuungana ili tuweze kujenga uchumi kwa ujumla,” alimaliza.
Stori: Neema Adrian | GPL