
LEO Jumamosi saa 10 jioni kwa saa za Tanzania, Simba SC itaikaribisha TP Mazembe ya DR Congo katika mchezo wake wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mechi hii ya kwanza kabla ya marudiano Aprili 13, mwaka huu huko Lubumbashi nchini DR Congo ni muhimu sana kwa Simba kupata ushindi ili kujiweka kwenye mazingira mazuri kabla ya kurudiana.
Pamoja na rekodi nzuri ya Simba kwenye mechi za kimataifa hasa inapokuwa nyumbani haipaswi kuingia uwanjani kwa kujiamini sana bali wanapaswa kujipanga na kwenda uwanjani kwa mipango madhubuti.
Ni vyema wachezaji wakiingia uwanjani wafahamu kwamba wana deni kubwa ambalo ni lazima walilipe kwa kupata ushindi hapa nyumbani hii leo. Ushindi kwenye mchezo huu utakuwa na maana kubwa kwao kwani watakuwa wametanguliza mguu mmoja mbele kwenda nusu fainali kabla ya mechi ya marudiano.
Hivyo ili kuwafanya Simba washinde mechi hii muhimu kwa taifa ni vyema mashabiki wakajitokeza kwa wingi ili kuwasapoti vijana wao ambao hata ukiangalia kwenye upangwaji wa ratiba walisema Simba ya kutoka nchini Tanzania.
Haitakuwa busara kuona Watanzania wanaenda Uwanja wa Taifa kuwashangilia wapinzani, litakuwa jambo la kushangaza hata wageni pia watatushangaa sana kwani mambo haya ni ya kizamani.
Kama Watanzania wote wataungana na kuishangilia Simba hakika wageni wanaweza kushangaa na kubabaika hali inayoweza kuwafanya wapoteze umakini ndani ya uwanja na hapo Simba watafanya kweli