MBUNGE wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba amemuambia Kocha Mkuu wa Yanga Mkongomani, Mwinyi Zahera ampe jina la mchezaji yeyote anayemuhitaji ili amsajili yeye.
Kauli hiyo, aliitoa juzi mkoani Dodoma kwenye uzinduzi wa uhamasishaji wa fedha zitakazotumika kwa ajili ya usajili wa Yanga.
Yanga hivi karibuni iliiteua Kamati Maalum ya Uhamasishaji wa Fedha iliyokuwa chini ya Naibu Waziri, Anthony Mavunde ambayo imepanga kukusanya shilingi bilioni 1.5. Tayari kamati hiyo imeanza kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa na mema yameanza kunukia Jangwani.
Zahera alisema, anamshukuru Mwigulu ambaye pia alimsajili kiungo wa Yanga, Feisal Salim ‘Fei Toto’ msimu uliopita.
Aliongeza kuwa, yeye tayari ana wachezaji kutoka nchi za Ghana, Mali wanaocheza nafasi ya beki, viungo na washambuliaji wenye gharama nafuu katika dau lao la usajili na mishahara.
“Ninashukuru kile nilichokuwa ninataka kinakwenda vizuri.
“Nilikutana na Mwigulu kabla ya uzinduzi huo kufanyika na kuzungumza naye vitu vingi kati ya hivyo ni kuniahidi kusajili mchezaji mmoja mimi ninayemuona mzuri, hivyo kilichobaki hivi sasa ni utekelezaji pekee,” alisema Zahera.
Wakati huohuo, neema inazidi kuongezeka Yanga baada ya Kamati ya Uhamasishaji kuahidi kuwalipa mishahara ya miezi sita wachezaji wake wote watakaosajiliwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.Kauli hiyo, aliitoa mwenyekiti wake Naibu Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde kwenye uzinduzi wa kamati hiyo huko mkoani Dodoma.
Kocha Mwinyi Zahera amesema viongozi hao wanataka kuona timu hiyo inajiendesha kisasa msimu ujao bila kumtegemea tajiri mmoja kama ilivyokuwa zamani.
Allipotafutwa Mavunde kuthibitisha hilo alikiri na kusema: “Fedha hizo tunazoendelea kuzichangisha zitasaidia kukiboresha kikosi pamoja na kupatikana fedha zitakazotumika kuwalipa mishahara ya miezi sita wachezaji wote tutakaowasajili.”
Kamati hiyo imepanga kukusanya kiasi cha bilioni 1.5 lakini inaonekana kiwango hicho kitazidi kutokana na kasi ya uchangiaji kuwa kubwa kufuatia juhudi kubwa inayofanywa na kamati iliyo chini ya Mavunde. Kwa siku moja tu ya juzi mkoani Dodoma, Sh milioni 500 z i l i kus anywa.
WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam