
KIKOSI cha Yanga leo kimebanwa mbavu na Mtibwa Sugar kwa kufungwa bao 1-0 kwenye mchezo wa ligi kuu uliochezwa Uwanja wa Jamhuri, mkoani Morogoro.
Yanga iliyo chini ya Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera imepoteza mchezo wake wa nne kwenye ligi kuu hali inayofanya ishindwe kuonyesha ushujaa kwa kuipiga nje ndani Mtibwa Sugar na kukubali kuwa dhaifu ugenini.
Kwa mara ya kwanza Yanga msimu huu walianza kupoteza mbele ya Stand United mkoani Shinyanga, wakapoteza mchezo wao wa pili mbele ya Simba uwanja wa Taifa pia walipoteza mbele ya Lipuli uwanja wa Samora na leo mbele ya Mtibwa Sugar.
Bao la Mtibwa Sugar lilipachikwa kimiani na mshambuliaji Riphat Khamis dakika ya 52 baada ya kutumia makosa ya beki Abdalah Shaibu ‘Ninja’ na kuachia mkwaju nje ya 18 uliomshinda Klaus Kindoki.
Jitihada za Yanga kuibuka na ushindi hazikuzaa matunda kwani dakika ya 85 walipata bao kupitia kwa Amis Tambwe ambaye mwamuzi alionyesha kwamba ameotea akimaliza pasi ya Mrisho Ngassa.
Ushindi huu unaifanya Yanga kuendelea kusalia kileleni ikiwa na pointi 74 baada ya kucheza michezo 32, huku Mtibwa Sugar wakibeba pointi tatu na kufikisha jumla ya pointi 48.