×

SIMBA NOMAA YAPINDUA MEZA KIBABE MBELE YA COASTAL UNION

SIMBA iliyo chini ya Kocha Mkuu Patrick Aussems, leo kwa mara ya kwanza kwenye Ligi Kuu Bara wamepindua meza kibabe baada ya kufungwa mapema na Razini Hafidh wa Coastal Union akimalizia mpira uliowachanganya wachezaji wa Simba, Aish Manula ambaye ni mlinda mlango na beki Erasto Nyoni dk ya 01.

Bao hilo lilidumu mpaka kipindi cha pili ambapo Simba walianza kuwanyua mashabiki dakika ya 49 kwa mkwaju wa penalti baada ya mchezaji wa Coastal Union kumchezea rafu Emanuel Okwi ndani ya 18 iliyozamishwa kimiani na Meddie Kagere.
Simba waliendelea kuonyesha utofauti wao licha ya kucheza kwenye uwanja wa Mkwakwani ambao ni kipara kwa kuwa hakuna majani sehemu kubwa ya uwanja na dakika ya 68 Kagere alirejea tena nyavuni akimaliza pasi mpenyezo ya Clatous Chama na kupachika bao la pili na la ushindi.
Ushindi huo unaifanya Simba kufikisha pointi 60 baada ya kucheza michezo 23 huku wakisalia kwenye nafasi yao ya tatu kwani kinara ni Yanga mwenye pointi 74 ambaye amecheza michezo 32.
Kwa msimu huu ni mara ya kwanza Simba kupindua matokeo kwani mchezo wa kwanza kupoteza walianza kufungwa na Mbao FC msimu uliopita dk ya 16 na Said Junior bao lililodumu mpaka dakika ya 90 Uwanja wa CCM Kirumba.