WANAFUKUA makaburi na kuzifanyia udhalilishaji maiti kwa sababu gani? Ni swali ambalo wengi wangetamani kupata majibu yake; ambapo UWAZI linakuja kufichua kilicho nyuma ya matukio ya aina hiyo.
Wiki iliyopita wananchi wa Jiji la Dar es Salaam walisikia au kushuhudia tukio lisilo la kawaida ambapo mwili wa aliyekuwa Ofisa wa Wizara ya Nishati, marehemu Mary Maramo (35), uliokuwa umezikwa katika makaburi ya Pugu Mwakanga jijini ulikutwa ukiwa umetolewa nje ya kaburi na kisha kuvuliwa nguo.
Tukio hilo ni mwendelezo wa mengine ya aina hiyo ambayo yamekuwa yakitokea sehemu mbalimbali nchini na kuacha sintofahamu mbele ya jamii.

TAFAKARI KABLA YA HABARI
Kumekuwa na taarifa mitaani kwamba kuna baadhi ya watu wamekuwa wakidiriki kuiingilia kimwili miili ya marehemu wa kike, jambo linaloacha maswali magumu juu ya kitendo hicho.
Katika dunia iliyojaa wanawake kila kona mwanaume rijali anawezaje kuivua nguo maiti na kuidhalilisha; kichwani anakuwa sawa au?
Kama hilo halitoshi kumekuwa na matukio ya watu kukata viungo vya maiti, kuchukua maji yaliyooshewa maiti na kukata viungo vya albino kwa madai ya kutukia kujipatia mali ambapo albino mmoja aliwahi kusema: “Nini viungo vyetu sisi wenyewe kwa miili yetu yote tukichimba madini hatupati sembuse wanaotukata mikono!”
MNAJIMU ANAFUNGUKA
Mnajimu maarufu Afrika Mashariki, Maalim Hassan Yahya Hussein (pichani) alipozungumza na gazeti hili jana na kuulizwa kuhusu vitendo hivyo alisema hufanywa na watu wenye imani za kishirikina.
“Tangu enzi na enzi, kuna imani potofu kwamba wenye kesi nzito kama vile za kuua au ufisadi mkubwa ambao mtuhumiwa anaona hawezi kunusurika huwa wanakwenda kwa waganga wa kienyeji na kudanganywa kwa kutumwa kuleta sanda, maji ya kuoshea maiti, nywele za maiti kwa madai kuwa kesi zao zitaisha,” alisema Maalim Hassan.
Akaongeza kuwa katika kazi yake ya unajimu inayomkutanisha na watu wengi ameshawahi kufikiwa na watu ambao walidai kuambiwa na waganga wapeleke viungo ili matatizo yao yaishe lakini walipofanya hivyo hayakuisha.
“Kuna wengine huwa wanakuja kwangu na kuniambia kuwa wamehangaika sana kwa waganga mpaka kupeleka maji ya kuoshea maiti lakini shida zao hazikuisha, mimi wakiniambia hivyo huwa nacheka na kuwaambia wanadanganywa kwa sababu maiti haiwezi kumaliza matatizo ya mtu aliye hai,” alisema.
Maalim Hassan aliongeza, vitendo vya ushirikina ni vibaya katika jamii na ndiyo maana hata baadhi ya watu wameshuhudiwa wakipelekwa mahakamani na kuhukumiwa kunyongwa kutokana na kukata viungo vya watu wenye ualbino.

USHUHUDA MZITO
Wakati UWAZI likifanya uchunguzi kujua kinachosababisha watu kufukua maiti na kuzifanyia udhalilisha, lilikutana na kijana mmoja (jina linahifadhiwa) ambaye mwaka 1998 alikumbwa na kesi ya wizi wa kutumia silaha.
“Kimsingi sikuwa mtu mzuri enzi hizo, nakumbuka mwaka huo tulikamatwa mimi na wenzangu watatu, tuwekwa mahabusu.
“Tulikaa mahabusu kama mwaka hivi, ndugu zetu wakaja na wazo kwamba wamekwenda kwa mganga na amewaambia tupeleke viungo vya maiti ili lifanyike zindiko kesi iiyeyuke.
“Wenzetu wawili walikuwa na uwezo wa kutoa fedha nakumbuka ilikuwa inahitajika kila mmoja wetu atoke laki tano ili viungo vipatikana pamoja na fedha za mganga.
“Mimi na mwenzangu hatukuwa safi lakini kwa kuwa tulikuwa tumechoka tukawaambia ndugu wauze mali zetu ili zindiko lifanywe, mke wangu alikataa kuuza kiwanja na boma langu la nyumba, nikakosa fedha za kufanyia zindiko,” alisema kijana huyo.
Aliongeza kuwa ndugu wa wenzake walifanikiwa kupata kiasi hicho na kwenda kufanya kafara jambo ambalo kijana huyo lilimuumiza kwa sababu aliona mkewe hakuwa na nia nzuri ya kumsaidia atoke gerezani.
Hata hivyo; baada ya kusota mahabusu kwa miaka mitatu na nusu kesi yao ilikuja kutolewa hukumu kwa wenzake watatu waliotoa kafara kuhukumiwa kifungo cha maisha jela na yeye kutoka kutokana na ushahidi wa kumtia hatiani kukosekana.
UCHUNGUZI MAKABURINI
Kufuatia tukio la hivi karibuni na kaburi la Mary kufukuliwa na mwili wake kufanyiwa unyama UWAZI lilifanya uchunguzi katika maeneo mbalimbali ya makaburi jijini Dar ili kujionea hali halisi ilivyo na hasa ulinzi.
Katika makaburi ya Kigilagila Kiwalani Mjumbe wa Serikali ya Mtaa huo, Julius Mahuna alisema kuwa katika makaburi hayo huwa kuna watu ambao wanakwenda kufanya matambiko japokuwa sasa matukio yanaonekana kupungua.
“Huwa kuna watu wanakuja hapa kufanya matambiko ya jadi, wengine huwa wanakuja kutupa vitu vya kiuganga. Huwa tunawafukuza kwa kutumia vijana maalum ambao huwa tunasaidiana kulinda makaburi haya.

“Kipindi cha nyuma kulikuwa na mbuyu mkubwa ambapo baadhi ya watu walikuwa wanakuja kufanya matambiko yao lakini kwa sasa umekatwa,” alisema kiongozi huyo.
Alipoulizwa kama katika eneo lake kuna maiti ziliwahi kufukuliwa alisema:
“Nakumbuka kuna wakati fulani watu walikuja ofisini kunitafuta wakiwa na vibali kuwa wanataka kuhamisha maiti yao kuipeleka mkoani, tukafuata utaratibu na hatimaye wakafukua na kuchukua mifupa na kuondoka nayo,” alisema kiongozi huyo.
UWAZI lilipofika katika makaburi Pugu Mwakanga alipozikwa Mary lilikuta ulinzi ukiwa umeimarishwa kutokana tukio ambalo limetokea.
Akizungumzia tukio la mwili wa Mary kufukuliwa, Mjumbe wa Shina namba 7 wa mtaa wa Bombani-Pugu Mwakanga alisema: “Ni kitu cha ajabu sijawahi kuona maishani mwangu. Nilishangaa kuona mwili umevuliwa nguo, hadi za ndani. Yaani binadamu tumekuwa wanyama kiasi hiki.”
MAKABURI YA KINONDONI
Kwenye makaburi ya Kinondoni umakini wa waangalizi wa makaburi ulikuwa umeongezeka ambapo mmoja wa wahusika aliyejitambulisha kwa jina moja la Jumbi alisema hakuna wa kufanya mchezo kwenye eneo hilo la makaburi.
“Ulinzi katika makaburi haya ni mkubwa achilia mbali kwamba hapa wanazikwa watu maarufu ikiwemo mastaa lakini leo (Jumapili) siyo siku ya kazi, njoo siku ya kazi watakuwepo wahusika wote hadi wachimbaji utapata taarifa zote ambazo unazihitaji,”alisema.
Baada hapo gazeti hili lilifunga safari mpaka makaburi ya Sinza ambapo lilikutana na kijana mmoja ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini akasema kwa sasa katika makaburi hayo haruhusiwi mtu yeyote kuingia kwa kuwa hawaziki tena.
WITO WA POLISI
Mara kadhaa jeshi la polisi linaloongozwa na IGP Simon Sirro kupitia vitengo vyake mbalimbali vimekuwa vikiwaelimisha watu kupuuza vitendo vya kishirikina kwani havina nafasi katika zama hivi za sayansi na teknolojia.
UTAPELI KUPITIA VIUNGO VYA MAITI
Chanzo kimoja cha habari kililiambia UWAZI kuwa matapeli wamekuwa wakitumia viungo vya binadamu kujipatia fedha kupitia kwa watu wanaotaka kupata utajiri wa njia za mkato.
“Siku za nyuma kulikuwa na kundi hatari sana jijini Dar, watu hawa walikuwa wanawaendea baadhi ya matajiri na kuwaambia watatajirika zaidi wakifanyiwa mambo ya kishirikina.
“Wale jamaa walikuwa wanakuambia utoe labda shilingi milioni kama 50 ili zifanyiwe dawa, baada ya siku saba utapata bilioni moja kwa kukuaminisha kwamba wanakupa labda hati yao ya nyumba ili usipopata uuze nyumba yao.
“Masharti ya dawa ni kupeleka viungo vya binadamu, ukiweza peleka ukiwa huwezi wao watakuja navyo, basi siku ya makabidhiano wakishachukua mwili na kukukabidhi viungo ili uvipeleke kwa mganga, wanawaita polisi wanakuja kukukamata na mkono wa binadamu na kujikuta unaishia jela maisha na wao wanaendelea na yao huku fedha wakiwa wamechukua.
Kuna watu wengi wako gerezani kutokana na kufanyiwa mchezo huo,” chanzo ambacho hakikutaka kuweka wazi jina kililiambia UWAZI wakati likifanya uchunguzi wa sababu za makaburi kufukuliwa.
Katika hatua nyingine watu wamewashauri wananchi ambao wanazika ndugu zao hasa kwenye makaburi ya kisasa ya kuweka mifuniko juu, kuchukua tahadhari ya kuhakikisha maiti za ndugu zao zinakuwa salama.
Aidha, wengine walisema kuwa tabia ya kuzika maiti ikiwa imevalishwa vitu vya thamani inatakiwa kuachwa kwa sababu huchangia makaburi kufukuliwa na wezi ili wazivue vito na nguo za gharama maiti.
Stori: ELVAN STAMBULI NA NEEMA ADRIAN, DAR