×

Zahera aishtaki Simba SC Caf

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera ni kama ameishtaki Simba kwa Shirikisho la Soka Afrika (Caf), baada ya kukutana nao na kuwaeleza namna ambavyo wapinzani wao hao walivyokuwa na viporo vingi katika Ligi Kuu Bara. Simba ambayo leo Jumatano inapambana na Coastal Union, ina mechi 16 mkononi kabla ya kumaliza msimu huu wa Ligi Kuu Bara, huku Yangaambayo nayo inacheza na Mtibwa Sugar leo, ina mechi saba.

 

Tofauti ya mechi za Simba na Yanga ni tisa kitu ambacho Zahera anaamini kinaweza kuifanya Simba kuwa bingwa kirahisi kutokana na kuwa na mechi nyingi mkononi zaidi yao licha ya kwamba wao wanaongoza ligi kwa sasa.

 

Katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, Yanga ikiwa imecheza mechi 31, inaongoza ikiwa na alama 74, huku Simba ikicheza mechi 22, inashika nafasi ya tatu na alama zake 57.

 

Hivi karibuni, Zahera alikutana na viongozi wa Caf ambao kwa sasa wapo jijini Dar wakifuatilia michuano ya vijana ya Kombe la Mataifa Afrika chini ya miaka 17 na kuwaeleza jambo hilo.

 

“Nilikutana na viongozi wa Caf wale waliokuja kwa ajili ya Afcon U-17, wakaniuliza namna gani tunaendelea na ligi, nikawaambia kuna timu moja hapa ina mechi 16 bado haijacheza na zingine zina mechi tano mpaka sita, walicheka sana,” alisema Zahera ambaye ni raia wa Ufaransa na DR Congo. Ishu ya Simba kuwa na viporo vingi imetokana na kushiriki kwao michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo wikiendi iliyopita waliondoshwa hatua ya robo fainali.