×

Hatimaye CCM Walitwaa Jimbo la Nassari

Mshindi wa ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), John Pallangyo.

 

MGOMBEA ubunge wa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), John Pallangyo,  amepita bila kupigwa katika nafasi hiyo baada ya wagombea wenzake 10 kushindwa kukidhi vigezo.

 

Msimamizi wa uchaguzi jimbo hilo, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru, Emmanuel Mkongo, amesema hayo  Ijumaa Aprili 19, 2019 wakati akitangaza matokeo baada ya upitiaji wa fomu zilizowasilishwa .

 

Mkongo amesema jumla ya wagombea 11 walichukua fomu na kati yao, watatu hawakurudisha na saba fomu zao zimebainika kutokidhi vigezo.

Amesema wapo ambao hawajalipa fedha ya dhamana ya kugombea ubunge ya Sh50,000, kukosa wadhamini na kurejesha fomu ya kiapo kutoka kwa mwanasheria na hakimu.

Akizungumza baada ya mkurugenzi kumtangaza kuwa kapita bila kupingwa, Pallangyo, amekishukuru chama chake kwa kumuamini na amesema atahakikisha anafuata nyayo za Rais John Magufuli katika utendaji kazi.

“Pia nitamkumbusha rais ahadi yake aliyoitoa ya ujenzi wa barabara ya kilometa tano za lami jimboni humo na nitahakikisha jimbo hilo linakuwa la mfano ndani ya muda mfupi,” amesema.