
MAMLAKA ya Hali ya Hewa nchini Tanzania (TMA) imetangaza kuwa Kimbunga Kenneth kimeongezeka kasi na kinatarajiwa kufika pwani ya kusini mwa Tanzania na kaskazini mwa Msumbiji kuanzia usiku wa Alhamisi wiki hii.
Kwa mujibu wa TMA, mpaka sasa (Jumatano mchana) kimbunga hicho kipo kilomita 450 kutoka pwani ya Mtwara na kina kasi ya kilomita 130 kwa saa.
Kufikia usiku wa leo, Aprili 24 kimpunga hicho kitakuwa kilomita 250 kutoka pwani ya Mtwara, kikiwa kinasafiri kwa kilomita 150 kwa saa.
Kimbunga hicho kinatarajiwa kuongeza nguvu zaidi Alhamisi mchana ambapo kitakuwa kinasafiri kwa kilomita 170 kwa saa na kitakuwa kilomita 150 kutoka pwani ya Mtwara.
Kwa mujibu wa TMA, eneo husika ambalo kimbunga hicho (landfall) litakuwa ni nchini Msumbiji, kikiwa na kasi ya kilomita 100 kwa saa. Eneo hilo litakuwa kilomita 200 kutoka pwani ya Mtwara.
Hata hivyo, mkoa wa Mtwara kwa upande wa Tanzania na maeneo jirani hususan mikoa ya Lindi na Ruvuma, athari zinategemewa kufikia umbali mpaka wa kilomita 500 kutoka Mtwara.
TMA imetahadharisha kuwa kimbunga hicho kitaingia nchi kavu na nguvu kubwa (ya upepo na mvua) itakayosababisha madhara makubwa kwa maisha ya watu na mali zao.
“Madhara yanayotarajiwa ni pamoja na mtawanyiko mkubwa wa mafuriko, uharibifu wa mali na makazi, kuezuliwa mapaa kutokana na upepo mkali na uharibifu wa mazao mashambani na miundombinu kutokana na mafuriko.” imeeleza taarifa iliyotolewa na TMA na kutaja madhara mengine kama: “Kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari katika kipindi kifupi (storm surge). Kuathirika kwa shughuli za usafirishaji kwa njia ya anga, kwenye maji na nchi kavu.”
Mtandao uliobobea kwenye masuala ya hali ya hewa wa AccuWeather wa nchini Marekani juzi ulikuwa wa kwanza kuripoti juu ya uwezekano wa kutokea kimbunga hicho. na kupiga maeneo ya kuanzia Lindi kusini mwa Tanzania mpaka Pemba kaskazini mwa Msumbiji.

Awali, Meneja wa Utabiri wa Hali ya Hewa wa Kimataifa wa AccuWeather, alitoa taarifa kuwa kimbunga Kenneth kinatarajiwa kuzikumba Tanzania na Msumbiji, Alhamisi usiku ama mapema Ijumaa wiki hii.
