Wizara ya Afya nchini Brazil imethibitisha jumla ya vifo 12,400 kutokana na #COVID19 huku idadi ya visa ikifika 178,214 na kuipita Ujerumani yenye visa 173,273 huku ikiwa inaikaribia Ufaransa yenye visa 178,228.
Baadhi ya nchi za Ulaya zinaanza kupunguza masharti ya zuio la kutotoka ndani, lakini mlipuko wa ugonjwa huo unazidi kuongezeka #Brazil ambapo Rais Jair Bolsonaro amewakosoa Magavana kwa kutoa amri ya watu kujitenga.
Wiki hii Rais Bolsonaro aliongeza mzozo baina yake na Magavana wa Majimbo baada ya kuainisha biashara kama Sehemu za Mazoezi (gyms) na saluni ni huduma muhimu hivyo zisizuiliwe.
Rais huyo amesema Magavana wasiokubaliana naye katika hilo wanaweza kwenda Mahakamani huku akiwatishia kuwa atachukua hatua za kisheria kwa wale wasiofuata maagizo yake.
Hata hivyo, takriban Magavana 10 wamesema hawatafuata agizo hilo. Gavana wa Rio de Janeiro, Wilson Witzel amesema “Bolsonaro anatembea kuelekea bondeni na anataka kutuchukua sisi wote pamoja naye.”
