×

Vladimir Putin, Kim Jong-un kuimrisha ushirikiano

 

KIONGOZI wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un, na rais wa Urusi, Vladimir Putin, wameahidi kuboresha mahusiano katika mkutano wao wa kwanza kuwahi kufanyika.

 

Wawili hao walisalimiana kwa kushikana mikono katika kisiwa cha Russky karibu na mji wa bandari wa Vladivostok, mashariki mwa Urusi.

 

Ikulu ya rais wa Urusi ya Kremlin imesema kuwa watajadili mpango wa kuacha matumizi ya zana za nuklia lakini Kim anasemekana pia yuko huko kuomba msaada baada ya mazungumzo na Marekani kutozaa matunda.

 

Rais wa Marekani Donald Trump na Kim walikutana Hanoi mapema mwaka huu lakini wakashindwa kufikia mapatano yoyote.

 

 

Kiongozi huyo wa Korea Kaskazini alikaribishwa kwa upendo na maofisa wa Urusi alipowasili Jumatano.  Kim alipokelewa kwa burudani ya bendi ya jeshi kabla ya kuingia ndani ya gari akiongozwa na walinzi wake ambao wamezoweleka sasa kwa kukimbia kando ya gari lake wakati linapoondoka.

 

“Nimewasili Urusi kwa moyo wa upendo wa watu wetu, na kama nilivyosema, natumaini ziara hii itakuwa ya mafanikio na ya maana,”  Kim alisema kwenye televisheni ya Urusi mapema baada ya kuvuka mpaka katika mji wa Khasan.

 

“Ni matumaini yangu kuwa wakati wa mazungumzo na rais anayeheshimika, Putin, nitaweza kujadili kwa kina masuala yanayohusiana na utatuzi wa suala la Tasi ya Korea, na kuendeleza mahusiano yetu ,” aliongeza.