×

Mch. Msigwa ‘Afukua Kaburi’ la Mawazo

MBUNGE  wa Iringa Mjini, Mch. Peter Msigwa,  amesema amesikitishwa na kauli ya Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe juu ya juhudi za kuwatafuta watu waliopotea.

 

Akichangia katika Bajeti ya Mambo ya Ndani, Msigwa amesema kwamba jeshi la polisi lenye dhamana ya kulinda raia na mali zake linapaswa kutoa ripoti ya wapi alipo mwandishi wa habari, Azory Gwanda, na si vinginevyo.

 

Amesema kwamba jeshi la polisi haliwezi kusifiwa kwa matukio kama hayo kwa kuwa uhai wa mtu ni wa thamani na Biblia inasema kwamba “Mtu mmoja akipotea taifa lazima linung’unike na watu wanaofariki siyo nzi”.

 

Ameendelea kusema kwamba: “Polisi imeshindwa kusema nani alimpiga risasi Lissu, aliyemuua Alphonce Mawazo, Ben Saanane yuko wapi, aliyemnyooshea risasi Nape aliyemteka Roma, lakini hata ripoti ya kutekwa kwa Mohammed Dewji mpaka leo haijatoka.”

 

Akikazia suala hilo, Msigwa amesema kazi ya Polisi ni kulinda raia na mali zao, na kwamba Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) aliahidi kulitolea ufafanuzi suala la utekwaji wa mfanyabiashara huyo baada ya rais kusema Watanzania siyo wajinga lakini mpaka sasa hakuna kilichoendelea.

 

“Polisi ina wajibu wa kusema kwa nini raia wanauawa kwa kuwa wao ndiyo wenye mabomu  na kila kitendea kazi. kazi yao ni kutulinda,” amesema.

 

Aidha amesema jeshi la polisi limekuwa likiwabambika na mbaya zaidi,  kwenye vituo vya polisi bado wanawafanyia raia unyanyasaji huku akibainisha kwamba hata yeye ameshwahi kuwa mhanga wa kutengenezewa kesi.