RAIS John Magufuli ametoa Tsh mil. 5 ili zisaidie katika ujenzi wa shule kijiji cha Charangwe mkoani Mbeya baada ya wananchi kujitolea kujenga madarasa ya shule hiyo.
Magufuli ametoa msaada huo leo Jumamosi, Aprili 27, 2019, alipokuwa akihutubia wananchi wa eneo hilo akipita kulekea wilayani Chunya mkoani humo ambako atakuwa na mkutano mkubwa na wananchi baadaye leo.
Aidha, amewapongeza wananchi hao kwa kujitolea kujenga madarasa na kituo cha afya kijijini hapo ambapo wamechangia kiasi cha shilingi milioni 70 huku serikali ikitoa shilingi milioni 500.
“Ninawapongeza sana wananchi wa Charangwe kwa kujitoa kwenu, sisi tumesema serikali yetu lazima itoe elimu bure, nyinyi mmekuwa mkijitoa kujenga madarasa, ninawaahidi serikali itaandelea kuwaunga mkono ili watoto wetu wapate elimu bila matatizo. Hiki kituo cha afya mlichojenga ninawaahidi nitaleta madaktari ili kianze kutumika,” amesema.
Mbali na hilo, ameagiza wachimbaji wadogo wasibughudhiwe katika eneo hilo kwani wana haki ya kuchimba madini ya nchi yao.