×

Simba Ilivyowashangaza Mbeya City Uwanja wa Sokoine (Picha +Video)

SIMBA hii unapokutana nayo ni lazima ujiandae kulia, yaani unapigwa unachakaa, maana moto wake si wa kitoto.

Jana Wekundu hao wa Msimbazi waliichapa Mbeya City mabao 2-1 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Sokoine jijini hapa.

Licha ya Mbeya City kutangulia kupata bao dakika ya 24 kupitia kwa Idd Nado, lakini hawakuambulia kitu katika mchezo huo, kwa kuwa Simba kama kawaida yao, waliamka mwishoni na kupata pointi tatu muhimu.

 

Kipindi cha kwanza kilimalizika, Mbeya City wakiwa wanaongoza kwa bao 1-0, na Yanga wakacheka sana, lakini Jonas Mkude akafunga bao la kusawazisha kwa kichwa dakika ya 67, kabla ya Meddie Kagere kufunga la pili dakika ya 84.

 

Simba wangeweza kupata bao la ushindi mapema, lakini Said Ndemla alikosa bao akiwa amebaki yeye na kipa dakika ya 70 baada ya shuti lake kwenda nje ya lango.

Matokeo hayo yameifanya Simba ifikishe jumla ya pointi 75, wakiwa wamebakiza pointi 5 tu waifikie Yanga lakini Simba wakiwa na viporo vya mechi tano kabla ya kufikia idadi ya mechi za Yanga.

 

Huu ni ushindi wa tano mfululizo wa Simba na sasa Wekundu hao wa Msimbazi wanaonekana watatangaza ubingwa mapema.

Baada ya kufungwa na Kagera 2-1, Simba imeshinda mechi tano mfululizo dhidi Alliance (2-0), KMC (2- 1), Biashara (2-0), JKT Tanzania (1-0) na Mbeya City (2-1).

Katika mechi hizo tano walizoshinda mfululizo, Simba wamefunga mabao ya ushindi kipindi cha pili kwenye mechi tatu, isipokuwa dhidi ya Biashara ambayo kipindi cha kwanza walikuwa wameshamaliza kazi na dhidi ya Alliance ambapo walikuwa wameshaongoza kipindi cha kwanza.

Katika mchezo wa jana, kipindi cha kwanza Simba walionekana kuwa na kasi ndogo huku Mbeya City wakifanya mashambulizi mengi, lakini kipindi cha pili Simba waliuchezea zaidi mpira wakitafuta bao la kusawazisha na la ushindi.

 

Dakika ya 30, beki wa Simba, Paul Bukaba aliumia na kumlazimisha kocha Patrick Aussems afanye mabadiliko ya lazima kwa kumuingiza Erasto Nyoni.

Kikosi cha Mbeya City kilichoanza dhidi ya Simba.

Kipindi cha pili, Aussems alimtoa Mohammed Ibrahim dakika ya 45 na nafasi yake kuchukuliwa na Emmanuel Okwi. Okwi aliwekwa nje katika mchezo huo, kwa kile kocha alichodai ni kuzungusha kikosi kutokana na mrundikano wa mechi nyingi ndani ya siku chache.

 

Kuonyesha kuwa kuna madhara ya kucheza mfululizo, Juuko Murshid wa Simba aliumia na nafasi yake ikachukuliwa na Yusuph Mlipili dakika ya 60.

Katika mchezo huo, kiungo matata Clatous Chama hakucheza kabisa kutokana na sababu hiyohiyo ya kocha kuzungusha kikosi.

 

Simba sasa inajiandaa na mchezo unaofuta dhidi ya Tanzania Prisons utakaochezwa kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, na kama wakishinda watakuwa wamebakiza pointi mbili tu kabla ya kuifikia Yanga.

PICHA/HABARI NA MUSA MATEJA | GPL