×

IGP Sirro: “Kama Kuna Mkono wa MTU, Sheria Itafuata Mkondo” – Video

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro (kushoto) akimfariji Abdiel Miku Mengi, mtoto wa marehemu Dr. Reginald Mengi, baada ya kusaini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa marehemu, Kinondoni jijini Dar es Salaam leo Mei 5, 2019..

 

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na Naibu Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba wamefika nyumbani kwa marehemu Dkt. Reginald Mengi, Kinondoni jijini Dar es Salaam kwa ajili kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu.

 

Akizungumza wakati akitoa pole hizo, IGP Sirro amesema; ”Mzee Mengi alikuwa mshauri mzuri sana kwenye masuala ya ulinzi na usalama pamoja na misaada midogomidogo kwa vijana wetu wanapokuwa na shida. Zaidi alikuwa ‘very humble’ (mnyenyekevu), mara zote alikuwa anajishusha sana. Mzee alikuwa ni mtu ambaye anaheshimu watu sana, jambo ambalo ni matajiri wachache wanakuwa hivyo.

 

Naibu Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba (kushoto) akisalimiana na Abdiel.

Sirro amesema kuwa Jeshi la Polisi limeona taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu kifo cha Mengi na tayari Jeshi linaanza kufanya uchunguzi na ili kubaini ukweli na maneno hayo. “Tumalize kwanza msiba….. hayo yanayozungumzwa mitandaoni tutafuatilia,” amesema Sirro.

 

Mzee Mengi alifariki dunia usiku wa kuamkia juzi Mei 2, 2019 nchini Dubai na mwili wake unatarajiwa kuwasili nchini Jumatatu, saa 8:00 mchana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam kabla ya kuagwa Karimjee, Posta, Jumanne, na kusafirishwa Jumatano kwenda nyumbani kwao Machame Kilimanjaro ambako utazikwa Alhamisi.