
BAWASIRI ni ugonjwa unaoibukia katika njia ya haja kubwa (rectum). Hujitokeza kama uvimbe au kijinyama ambacho huweza kuonekana hadi nje.
Kwa Kiingereza hujulikana kama haemorrhoids au piles. Uvimbe hutokea kwa ndani na kwa nje ya njia ya haja kubwa.
Bawasiri inaweza kusababisha upungufu wa damu mwilini na inaweza kutibika ama kwa upasuaji au kwa matumizi ya dawa mbadala kwa kipindi kirefu kama wiki sita au hata zaidi kutegemea ilikuwa imejijenga namna gani. Hakuna sababu ya moja kwa moja inayojulikana kisayansi kwamba ndiyo husababisha bawasiri, bali mambo yafuatayo yanaweza kusababisha kupatwa na ugonjwa huu:
Mosi; kufunga choo au kupata choo kigumu kwa muda mrefu, pili; ujauzito – wakati wa ujauzito watu wengine wanaweza kupatwa na bawasiri kwa sababu ya msukumo wa mtoto karibu na sehemu ya kutolea haja kubwa na tatu; kushiriki mapenzi kinyume na maumbile. Sababu nyingine ni za kurithi.
Baadhi ya watu wanaweza kurithi udhaifu wa ukuta huo wa njia ya haja ya kubwa ingawa ni asilimia ndogo sana, kuharisha sana kwa muda mrefu, kunyanyua vyuma vizito, mfadhaiko/stress, kuwa na uzito mkubwa na unene kupita kiasi ni moja ya sababu ya kupata ugonjwa huu.

DALILI ZAKE
Dalili zipo nyingi kama vile mgonjwa kujisikia maumivu wakati wa kujisaidia haja kubwa, kinyesi kuwa na damu wakati wa kujisaidia, muwasho sehemu ya tundu la haja kubwa, uvimbe au kinyama kujitokeza sehemu ya tundu la haja kubwa na haja kubwa yaweza kujitokea tu muda wowote.
MADHARA YA BAWASIRI
Madhara makubwa ni maumivu na mgonjwa kupata upungufu wa damu (anemia), kupata tatizo la kutokuweza kuhimili choo, hupunguza nguvu za kiume na kuondoa hamu ya tendo la ndoa kwa wanawake na kuathirika kisaikolojia.
Bawasiri ni ugonjwa unaoanzia ndani ya tumbo kwenye mfumo wako wa mmeng’enyo wa chakula. Ukiugua bawasiri ujue kuna kitu si sawa ndani ya tumbo lako. Bawasiri ni ishara ya moja kwa moja kwamba kwenye mfumo wako wa mmeng’enyo wa chakula kuna tatizo.
MATIBABU NA USHAURI
Ukiwa na dalili tulizozitaja onana na daktari wako au mtaalamu, atakupa dawa stahiki au atakufanyia upasuaji kama hapana budi. Ushauri mwingine ni kwamba unahitaji kula chakula chenye vitamini nyingi za kutosha ambazo ni muhimu kwa afya ya mwili. Watanzania wengi wanaugua bawasiri kutokana na sababu kuu mbili, moja; wanakula ugali wa sembe badala ya ugali wa dona, pili hawanywi maji ya kutosha kila siku na wengine hawanywi maji mpaka wasikie kiu.