
SERIKALI imependekeza kupandisha kwa ushuru wa asilimia 10 kwa bidhaa za nywele bandia zinazozalishwa nchini na asilimia 25 kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje nchi.
Pendekezo hilo limetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dr Philip Mpango, wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
“Napendekeza kutoza ushuru wa asilimia 10 kwenye bidhaa za nywele za bandia, zinazotengenezwa ndani ya nchi na asilimia 25 zinazoagizwa kutoka nje ya nchi, lengo ni kuongeza mapato ya Serikali,” alisema na kuongeza:
“Napendekeza kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye makasha yenye majokofu yanayotumika kwenye kilimo cha kisasa cha mbogamboga kwa wakulima watakaoingiza makasha hayo kutoka nje ya nchi kwa matumizi ya kilimo.
Pia, alipendekeza kuongeza muda wa leseni ya udereva kutoka miaka mitatu hadi mitano, kuongeza tozo ya leseni 40,000 hadi 70,000, ada ya usajili wa magari 10,000 hadi 50,000, Bajaj kutoka 10,000 hadi 30,000 na pikipiki kutoka 10,000 hadi 20,000.
Mengine yaliyotolewa kama mapendekezo ni kutoza ushuru wa asilimia 35 badala ya 25 kwa mwaka mmoja kwenye bidhaa za soseji na zinazofanana na hizo, pia kutoza kodi ya asilimia 35 badala ya 25 kwa nyanya zilizosindikwa (tomato sauce).
Baada ya waziri kuwasilisha pendekezo hilo kwenye bajeti ya Serikali, ukumbi wa Bunge ulilipuka kwa kelele kwa wabunge wakipiga meza zao wakionyesha kufurahia pendekezo hilo.
Aidha katika bajeti, waziri alipendekeza kupandishwa tozo leseni ya magari ya pamoja na kuongeza miaka kutoka miaka mitatu hadi miaka mitano, kwa mwaka 2018/2019.