
Mkuu wa majeshi wa Ethiopia Searre Mekonnen, ameuawa kwa kupigwa risasi na mlinzi wake. Msemaji wa waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, Billene Seyoum amesema leo kwamba mkuu huyo wa majeshi aliuawa saa chache baada ya jaribio la mapinduzi, katika jimbo la Amhara.
Kwenye jaribio hilo, rais wa jimbo hilo aliuawa pamoja na afisa mwengine ambaye ni mshauri mkuu wa rais wa jimbo hilo. Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ametangaza kwa njia ya televisheni kuwa serikali yake imevunja jaribio hilo la mapinduzi.
Billene Seyoum amewaambia waandishi wa habari kuwa watu aliowaita kuwa ‘mamluki’ walioongozwa na mkuu wa usalama wa jimbo la Amhara Asamnew Tsige, walishambulia mkutano na kumjeruhi rais wa jimbo hilo Ambachew Mekonnen na afisa mwengine.
Wote wawili tayari wamekufa kutokana na majeraha waliyoyapata.
Baadaye kulikuwa na kile Billene amekieleza kuwa shambulizi la kupangwa katika ofisi ya mkuu wa majeshi ambapo mkuu huyo wa majeshi aliuawa.