
PATRICK Aussems, Kocha Mkuu wa Simba, ameamua kuwapa dakika 360 wachezaji wake wapya wakiongozwa na Wabazil watatu ili kuona uwezo wao halisi ndani ya uwanja.
Simba ikiwa nchini Afrika Kusini itacheza michezo minne ya kirafiki kwa ajili ya kukiandaa kikosi cha ushindani msimu ujao huku dakika hizo walengwa
wakubwa wakitajwa kuwa ni wachezaji hao watatu raia wa Brazil.
Wilker Henrique da Silva, Gerson Fraga Viera, Tairone da Silva, hawa ni raia wa Brazil waliosaini kandarasi ya miaka miwili, Sharaf Eldin Shiboub Ali Abdalrahman raia wa Sudan amesaini kandarasi ya mwaka mmoja. Wengine ni Francis Kahata, Deo Kanda, Ibrahim Ajibu, Gadiel Michael, Miraj Athuman na Beno Kakolanya, haya ni maingizo mapya.
Akizungumza na Championi Jumatatu, mlinda mlango mpya Beno Kakolanya amesema kuwa maandalizi yanakwenda sawa na mechi watakazocheza zitawajengea hali ya kujiamini. “Tupo vizuri na maandalizi yanakwenda sawa, ni wakati wa kuunda kikosi imara kwa ajili ya ushindani msimu ujao,” alisema Kakolanya.